Amu. 19:1-12 Swahili Union Version (SUV)

1. Ikawa katika siku hizo, hapo kulipokuwa hapana mfalme katika Israeli, alikuwapo Mlawi mmoja aliyekuwa akikaa hali ya ugeni upande wa mbele wa nchi ya vilima vilima ya Efraimu, aliyejitwalia suria katika Bethlehemu-yuda.

2. Kisha huyo suria yake akaandama ukahaba kinyume chake, kumwacha kwenda nyumbani kwa baba yake huko Bethlehemu-yuda, akakaa kuko muda wa miezi minne.

3. Kisha mumewe akainuka akamfuata, aseme naye kwa upendo, ili apate kumrudisha tena, naye alikuwa na mtumishi wake pamoja naye na punda wawili; huyo mwanamke akamkaribisha katika nyumba ya baba yake; naye baba yake alipomwona akafurahi kuonana naye.

4. Kisha mkwewe, babaye huyo mwanamke, akamzuia; akakaa naye siku tatu; basi wakala na kunywa na kulala kuko.

5. Kisha ilikuwa siku ya nne, wakaamka asubuhi na mapema, naye akaondoka ili aende zake; baba yake huyo mwanamke akamwambia mkwewe, Tuza moyo wako, ule chakula kidogo, kisha baadaye mtakwenda zenu.

6. Basi wakaketi, wakala na kunywa wote wawili pamoja; kisha baba yake mwanamke akamwambia huyo mtu, Uwe radhi, tafadhali, ukae usiku kucha, na moyo wako na ufurahi.

7. Yule mtu akainuka ili aondoke; lakini mkwewe akamsihi-sihi, naye akalala kuko tena.

8. Basi akaamka asubuhi na mapema siku ya tano ili aende zake; na baba yake mwanamke akasema, Tuza moyo wako, tafadhali, ukae hata jua lipinduke; nao wakala chakula wote wawili.

9. Kisha hapo mtu huyo alipoinuka ili aende zake, yeye na suria yake, na mtumishi wake, huyo mkwewe, baba yake mwanamke, akamwambia, Tazama mchana wakaribia jioni, tafadhali kaa usiku kucha; tazama mchana wakaribia mwisho wake, lala hapa, ili moyo wako ufurahi; hata kesho uende zako asubuhi na mapema, ili upate kwenda kwenu.

10. Lakini huyo mtu hakukubali kukaa usiku huo, ila akainuka, akaenda zake, akafika mkabala wa Yebusi (huo ndio Yerusalemu); nao walikuwako pamoja naye punda wawili waliotandikwa; suria yake naye alikuwa pamoja naye.

11. Basi hapo walipokuwa karibu na Yebusi, mchana ulikuwa umeendelea mno; yule mtumishi akamwambia bwana wake, Haya, tafadhali, tugeuke kando na kuingia mji huu wa Wayebusi, tulale humu.

12. Bwana wake akamwambia, Hatutageuka sisi kuingia mji wa wageni, ambao si wa wana wa Israeli; lakini tutapita mpaka Gibea.

Amu. 19