Amu. 16:17-28 Swahili Union Version (SUV)

17. Ndipo alipomwambia yote yaliyokuwa moyoni mwake, akamwambia, Wembe haukupita juu ya kichwa changu kamwe; maana mimi nimekuwa Mnadhiri wa Mungu, tangu tumboni mwa mama yangu; nikinyolewa, ndipo nguvu zangu zitanitoka, nami nitakuwa dhaifu, nitakuwa kama wanadamu wenzangu.

18. Delila alipoona ya kuwa amemwambia yote yaliyokuwa moyoni mwake, akatuma mtu akawaita wakuu wa Wafilisti, akisema, Njoni huku mara hii tu, maana ameniambia yote aliyo nayo moyoni mwake. Ndipo wakuu wa Wafilisti wakamwendea wakachukua ile fedha mikononi mwao.

19. Naye akamlaza usingizi magotini pake. Kisha akamwita mtu akavinyoa vile vishungi saba vya nywele za kichwa chake; akaanza kumsumbua, nguvu zake zikamtoka.

20. Kisha akasema, Samsoni, Wafilisti wanakujia. Akaamka katika usingizi wake, akasema, Nitakwenda nje kama siku nyingine, na kujinyosha. Lakini hakujua ya kuwa BWANA amemwacha.

21. Wafilisti wakamkamata, wakamng’oa macho; wakatelemka naye mpaka Gaza, wakamfunga kwa vifungo vya shaba; naye alikuwa akisaga ngano katika gereza.

22. Lakini zile nywele za kichwa chake zikaanza kukua tena baada ya kunyolewa kwake.

23. Kisha wakuu wa Wafilisti wakakusanyika ili kumtolea sadaka Dagoni mungu wao, na kufurahi; maana walisema, Mungu wetu amemtia Samsoni adui wetu mikononi mwetu.

24. Na hao watu walipomwona wakamhimidi mungu wao, maana walisema, Mungu wetu amemtia mikononi mwetu huyu adui wetu, aliyeiharibu nchi yetu na kuwaua watu wengi miongoni mwetu.

25. Ikawa mioyo yao iliposhangilia, wakasema, Mwiteni Samsoni, ili atufanyie michezo. Basi wakamwita Samsoni atoke gerezani, akacheze mbele yao wakamweka katikati ya nguzo mbili.

26. Samsoni akamwambia yule kijana aliyemshika mkono, Niache nizipapase nguzo ambazo nyumba hii inazikalia, nipate kuzitegemea.

27. Basi nyumba ile ilikuwa imejaa watu waume kwa wake; na wakuu wote wa Wafilisti walikuwamo humo, na juu ya dari palikuwa na watu elfu tatu waume kwa wake waliokuwa wakitazama, wakati Samsoni alipocheza.

28. Samsoni akamwita BWANA, akasema, Ee Bwana MUNGU, unikumbuke, nakuomba, ukanitie nguvu, nakuomba, mara hii tu, Ee Mungu, ili nipate kujilipiza kisasi juu ya Wafilisti kwa ajili ya macho yangu mawili.

Amu. 16