11. Akamwambia Wakinifunga tu kwa kamba mpya ambazo mtu hakufanya kazi nazo, hapo ndipo nitakuwa dhaifu, nitakuwa kama wanadamu wenzangu.
12. Basi Delila akatwaa kamba mpya akamfunga nazo, akamwambia, Wafilisti wanakujia, Samsoni. Na wale wenye kuotea walikuwa katika chumba cha ndani. Naye akazikata, akazitupa kutoka mikononi mwake kama uzi.
13. Delila akamwambia Samsoni, Hata sasa umenidhihaki, umeniambia maneno ya uongo; niambie sasa, waweza kufungwa kwa kitu gani? Akamwambia, Ukivifuma hivi vishungi saba vya nywele za kichwa changu katika mtande wa nguo.
14. Basi akazifunga kwa msumari, akamwambia Samsoni, Wafilisti wanakujia. Naye akaamka usingizini, akaung’oa ule msumari, na ule mtande.
15. Mwanamke akamwambia, Wawezaje kusema, Nakupenda; na moyo wako haupo pamoja nami? Umenidhihaki mara hizi tatu, wala hukuniambia asili ya nguvu zako nyingi.
16. Ikawa, kwa vile alivyomsumbua kwa maneno yake kila siku, na kumwudhi, roho yake ikadhikika hata kufa.
17. Ndipo alipomwambia yote yaliyokuwa moyoni mwake, akamwambia, Wembe haukupita juu ya kichwa changu kamwe; maana mimi nimekuwa Mnadhiri wa Mungu, tangu tumboni mwa mama yangu; nikinyolewa, ndipo nguvu zangu zitanitoka, nami nitakuwa dhaifu, nitakuwa kama wanadamu wenzangu.
18. Delila alipoona ya kuwa amemwambia yote yaliyokuwa moyoni mwake, akatuma mtu akawaita wakuu wa Wafilisti, akisema, Njoni huku mara hii tu, maana ameniambia yote aliyo nayo moyoni mwake. Ndipo wakuu wa Wafilisti wakamwendea wakachukua ile fedha mikononi mwao.
19. Naye akamlaza usingizi magotini pake. Kisha akamwita mtu akavinyoa vile vishungi saba vya nywele za kichwa chake; akaanza kumsumbua, nguvu zake zikamtoka.
20. Kisha akasema, Samsoni, Wafilisti wanakujia. Akaamka katika usingizi wake, akasema, Nitakwenda nje kama siku nyingine, na kujinyosha. Lakini hakujua ya kuwa BWANA amemwacha.