12. Manoa akasema, Basi sasa hayo maneno yako yatakapotimia, je! Huyo mtoto atakuwa wa namna gani, na kazi yake itakuwa ni nini?
13. Malaika wa Mungu akamwambia Manoa, Katika hayo yote niliyomwambia huyo mwanamke na ajihadhari.
14. Asile kitu cho chote kitokacho katika mzabibu, wala asinywe divai, wala mvinyo, wala asile kitu cho chote kilicho najisi; hayo yote niliyomwamuru na ayatunze.
15. Kisha Manoa akamwambia huyo malaika wa BWANA, Nakuomba, tukuzuie, ili tupate kuandaa mwana-mbuzi kwa ajili yako.
16. Lakini malaika wa BWANA akamwambia Manoa, Ujapokuwa wanizuia, sitakula katika mkate wako; na kwamba wataka kufanya tayari sadaka ya kuteketezwa, inakupasa kumsongezea BWANA. Kwa kuwa Manoa hakujua ya kwamba yeye ni malaika wa BWANA.
17. Manoa akamwambia huyo malaika wa BWANA, Jina lako ni nani, ili kwamba hapo hayo maneno yako yatakapotimia nipate kukutukuza?
18. Huyo malaika wa BWANA akamwambia, Kwani wewe kuniuliza jina langu, kwa kuwa jina hilo ni la ajabu?
19. Basi Manoa akamtwaa yule mwana-mbuzi, pamoja na sadaka ya unga, akamtolea BWANA hapo juu ya mwamba; huyo malaika akatenda la ajabu; Manoa na mkewe wakaangalia.
20. Kwa maana, ikawa, mara huo mwali wa moto ulipopaa juu mbinguni kutoka pale madhabahuni, huyo malaika wa BWANA akapaa katika mwali wa moto wa madhabahu; nao Manoa na mkewe wakaangalia; wakainama kifudifudi.