22. Nao wakaumiliki mpaka wote wa Waamori, tokea Arnoni hata Yaboki, tokea hiyo bara hata Yordani.
23. Basi sasa yeye BWANA, Mungu wa Israeli, amewapokonya Waamori watoke mbele ya watu wake Israeli, na wewe wataka kuwatamalaki?
24. Je! Wewe hutakitamalaki hicho ambacho huyo Kemoshi mungu wako akupa kukitamalaki? Kadhalika, awaye yote ambaye BWANA, Mungu wetu, amemfukuza atoke mbele yetu hao ndio tutakaowatamalaki.
25. Na wewe sasa, je! U mwema kuliko Balaki mwana wa Sipori, huyo mfalme wa Moabu, kwa lo lote? Je! Yeye alishindana na Israeli, au kupigana nao?
26. Wakati Israeli waliokuwa wakikaa Heshboni na miji yake, na katika Aroeri na miji yake, na katika miji hiyo yote iliyo huko kando ya Arnoni, muda wa miaka mia tatu; mbona ninyi hamkuipata tena katika majira hayo?
27. Basi mimi sikukufanyia wewe dhambi, lakini wewe unanitenda uovu kwa kupigana nami; yeye BWANA, yeye Mwamuzi, na awe mwamuzi hivi leo kati ya wana wa Israeli na wana wa Amoni.
28. Lakini mfalme wa wana wa Amoni hakuyasikiza hayo maneno ya Yeftha aliompelekea.
29. Ndipo roho ya BWANA ikamjilia juu yake Yeftha, naye akapita katika Gileadi na Manase, akapita na katika Mispa ya Gileadi, na kutoka hapo Mispa ya Gileadi akapita kuwaendea wana wa Amoni.
30. Naye Yeftha akamwekea BWANA nadhiri, akasema, Kwamba wewe utawatia wana wa Amoni mkononi mwangu kweli,
31. ndipo itakuwa ya kwamba, kile kitakachotoka katika milango ya nyumba yangu kunilaki, hapo nitakaporudi na amani kutoka kwa hao wana wa Amoni, kitu hicho kitakuwa ni cha BWANA, nami nitakisongeza kiwe sadaka ya kuteketezwa.