Amu. 11:15-23 Swahili Union Version (SUV)

15. akamwambia, Yeftha akuambia hivi; Israeli hakuitwaa nchi ya Moabu, wala nchi ya wana wa Amoni;

16. lakini hapo walipokwea kutoka Misri, na Israeli walienenda katika bara hata kuifikilia Bahari ya Shamu, na kufikilia Kadeshi;

17. ndipo Israeli wakatuma wajumbe waende kwa mfalme wa Edomu, wakisema, Nakuomba sana unipe ruhusa nipite katika nchi yako; lakini mfalme wa Edomu hakusikia. Ni vivyo wakampelekea wajumbe mfalme wa Moabu; wala yeye hakukubali; basi Israeli wakakaa katika Kadeshi.

18. Kisha akaenda nyikani na kuizunguka hiyo nchi ya Edomu, na nchi ya Moabu, nao wakapita upande wa mashariki wa nchi ya Moabu, wakapanga marago upande wa pili wa Arnoni; wala hawakuingia ndani ya mpaka wa Moabu, kwa maana Arnoni ilikuwa ni mpaka wa Moabu.

19. Kisha Israeli wakatuma wajumbe waende kwa Sihoni mfalme wa Waamori, mfalme wa Heshboni: Israeli wakamwambia, Twakuomba utupe ruhusa tupite katika nchi yako, mpaka mahali pangu.

20. Lakini huyo Sihoni hakuwaamini Israeli ili wapite ndani ya mpaka wake; bali Sihoni akawakutanisha watu wake wote, nao wakapanga kambi katika Yahasa, wakapigana na Israeli.

21. BWANA, Mungu wa Israeli, akamtia Sihoni na watu wake wote mikononi mwa Israeli, nao wakawapiga; basi Israeli wakaimiliki hiyo nchi ya Waamori, wenye kukaa nchi hiyo.

22. Nao wakaumiliki mpaka wote wa Waamori, tokea Arnoni hata Yaboki, tokea hiyo bara hata Yordani.

23. Basi sasa yeye BWANA, Mungu wa Israeli, amewapokonya Waamori watoke mbele ya watu wake Israeli, na wewe wataka kuwatamalaki?

Amu. 11