4. Huyo alikuwa na wana thelathini waliokuwa wakipanda wana-punda thelathini, nao walikuwa na miji thelathini, ambayo inaitwa Hawoth-yairi hata hivi leo, nayo iko katika nchi ya Gileadi.
5. Yairi akafa, akazikwa huko Kamoni.
6. Kisha wana wa Israeli walifanya tena yaliyo maovu mbele za macho ya BWANA, wakawatumikia Mabaali, na Maashtorethi, na miungu ya Shamu, na miungu ya Sidoni, na miungu ya Moabu, na miungu ya wana wa Amoni, na miungu ya Wafilisti; nao wakamwacha BWANA, wala hawakumtumikia yeye.
7. Hasira za BWANA ziliwaka juu ya Israeli, akawauza na kuwaua mikononi mwa Wafilisti, na mikononi mwa wana wa Amoni.
8. Nao wakawasumbua na kuwaonea wana wa Israeli mwaka huo; waliwaonea wana wa Israeli wote waliokuwa ng’ambo ya pili ya Yordani katika nchi ya Waamori, iliyoko huko Gileadi, muda wa miaka kumi na minane.
9. Wana wa Amoni nao wakavuka Yordani ili wapigane na Yuda, na kupigana na Benyamini, na nyumba ya Efraimu; basi hivyo Israeli walikuwa wanasumbuliwa sana.
10. Ndipo wana wa Israeli wakamlilia BWANA, wakisema, Sisi tumekufanyia dhambi, kwa sababu tumemwacha Mungu wetu, na kuyatumikia Mabaali.
11. Naye BWANA akawaambia wana wa Israeli, Je! Sikuwaokoa ninyi na hao Wamisri, na Waamori, na wana wa Amoni, na Wafilisti?
12. Hao Wasidoni nao, na Waamaleki, na Wamaoni, waliwaonea, nanyi mlinililia, nami niliwaokoa na mikono yao.
13. Lakini mmeniacha mimi, na kuitumikia miungu mingine; basi kwa ajili ya hayo mimi sitawaokoa tena.
14. Haya, endeni mkaililie hiyo miungu mliyoichagua; na hiyo iwaokoe wakati wa kusumbuka kwenu.
15. Wana wa Israeli wakamwambia BWANA Tumefanya dhambi; utufanyie yote uyaonayo kuwa ni mema; lakini tuokoe, twakusihi, siku hii ya leo, haya tu.
16. Nao wakaiondoa hiyo miungu ya kigeni iliyokuwa kati yao, nao wakamtumikia BWANA; na roho yake ilihuzunika kwa sababu ya msiba wa Israeli.