Amo. 2:1-8 Swahili Union Version (SUV)

1. Haya ndiyo asemayo BWANA; Kwa makosa matatu ya Moabu, naam, kwa manne, sitaizuia adhabu yake isimpate; kwa sababu aliichoma moto mifupa ya mfalme wa Edomu hata ikawa chokaa; Sef 2:8-11; 2 Fal 3:27

2. lakini nitapeleka moto juu ya Moabu, nao utayateketeza majumba ya Keriothi; na Moabu atakufa pamoja na mshindo, na kelele, na sauti ya tarumbeta;

3. nami nitamkatilia mbali mwamuzi atoke kati yake, nami nitawaua wakuu wake pamoja naye, asema BWANA.

4. Haya ndiyo asemayo BWANA; Kwa makosa matatu ya Yuda, naam, kwa manne, sitaizuia adhabu yake isimpate; kwa sababu wameikataa sheria ya BWANA; wala hawakuzishika amri zake; na maneno yao ya uongo yamewakosesha, ambayo baba zao waliyafuata;

5. lakini nitapeleka moto juu ya Yuda, nao utayateketeza majumba ya Yerusalemu.

6. Haya ndiyo asemayo BWANA; Kwa makosa matatu ya Israeli, naam, kwa manne, sitaizuia adhabu yake isimpate; kwa sababu wamewauza wenye haki kwa fedha, na maskini kwa jozi ya viatu;

7. nao hutwetea mavumbi yaliyo juu ya vichwa vya maskini, na kuipotosha njia ya mwenye upole; na mtu na baba yake humwendea mwanamke mmoja, hata kulitia unajisi jina langu takatifu;

8. nao hujilaza karibu na kila madhabahu juu ya nguo zilizowekwa rehani, na katika nyumba ya Mungu wao hunywa divai ya watu waliotozwa fedha.

Amo. 2