7. Lakini Daudi aliipiga ngome ya Sayuni; huu ndio mji wa Daudi.
8. Naye Daudi alisema siku hiyo, Yeye atakayewapiga Wayebusi, na apande kwenye mfereji wa maji, na kuwapiga viwete, na hao vipofu, ambao roho yake Daudi inawachukia. Kwa sababu hii watu husema, Wako vipofu na viwete hawawezi kuingia nyumbani.
9. Basi Daudi akakaa ndani ya ngome hiyo, akaiita mji wa Daudi. Kisha Daudi akajenga toka Milo na pande za ndani.
10. Naye Daudi akazidi kuwa mkuu; kwa maana BWANA, Mungu wa majeshi, alikuwa pamoja naye.
11. Kisha Hiramu, mfalme wa Tiro, akatuma wajumbe kwa Daudi, akampelekea na mierezi, na maseremala, na waashi; nao wakamjengea Daudi nyumba.
12. Akajua Daudi ya kwamba BWANA amemweka imara awe mfalme juu ya Israeli, na ufalme wake ameutukuza kwa ajili ya watu wake, Israeli.
13. Naye Daudi akazidi kujitwalia masuria na wake huko Yerusalemu baada ya kutoka Hebroni; wakazaliwa zaidi kwa Daudi wana na binti.
14. Na haya ndiyo majina ya hao waliozaliwa kwake huko Yerusalemu; Shamua, na Shobabu, na Nathani, na Sulemani,
15. na Ibhari, na Elishua; na Nefegi, na Yafia;
16. na Elishama, na Eliada, na Elifeleti.
17. Na hao Wafilisti waliposikia kwamba wamemtia Daudi mafuta ili awe mfalme juu ya Israeli, Wafilisti wote wakapanda kumtafuta Daudi; naye Daudi akapata habari, akashuka akaenda ngomeni.
18. Basi Wafilisti walikuwa wamekuja na kujitawanya bondeni mwa Warefai.
19. Basi Daudi akauliza kwa BWANA, akisema, Je! Nipande juu ya Wafilisti? Utawatia mkononi mwangu? Naye BWANA akamwambia Daudi, Panda; kwa kuwa hakika nitawatia Wafilisti mikononi mwako.
20. Basi Daudi akaja Baal-perasimu, naye Daudi akawapiga huko; akasema, BWANA amewafurikia adui zangu mbele yangu, kama mafuriko ya maji. Basi akapaita mahali pale Baal-perasimu.
21. Nao wakaziacha sanamu zao huko, na Daudi na watu wake wakaziondolea mbali.