25. Basi ikawa, alipofika Yerusalemu kumlaki mfalme, mfalme akamwambia, Mbona hukwenda pamoja nami, Mefiboshethi?
26. Naye akajibu, Bwana wangu, Ee mfalme, mtumwa wangu alinidanganya; kwa kuwa mimi mtumwa wako nilisema, Nitajitandikia punda, nipate kumpanda, na kwenda pamoja na mfalme; kwa sababu mimi mtumwa wako ni kiwete.
27. Naye amenisingizia mimi mtumwa wako kwa bwana wangu mfalme; lakini bwana wangu mfalme ni kama malaika wa Mungu; utende basi yaliyo mema machoni pako.
28. Kwa kuwa jamaa yote ya baba yangu walikuwa kama watu wa kufa tu mbele ya bwana wangu mfalme; ila uliniweka mimi mtumwa wako kati ya hao walao mezani pako. Basi ni haki gani sasa niliyo nayo, hata nimlilie mfalme zaidi?
29. Basi mfalme akamwambia, Kwa nini unazidi kuyanena mambo yako? Mimi naamua, Wewe na Siba mwigawanye hiyo nchi.
30. Naye Mefiboshethi akamwambia mfalme, Naam, hata yote na atwae yeye, kwa kuwa bwana wangu mfalme amekuja kwa amani nyumbani kwake.
31. Tena Barzilai, Mgileadi, akashuka kutoka Rogelimu; akavuka Yordani pamoja na mfalme, amvushe Yordani.
32. Naye huyo Barzilai alikuwa mzee sana, amepata umri wa miaka themanini; naye amemlisha mfalme hapo alipokuwapo Mahanaimu; kwa kuwa alikuwa mtu mwenye cheo kikubwa.
33. Naye mfalme akamwambia Barzilai, Uvuke pamoja nami; nami nitakulisha kwangu huko Yerusalemu.
34. Lakini Barzilai akamjibu mfalme, Siku ni ngapi za miaka ya maisha yangu, hata mimi nipande pamoja na mfalme kwenda Yerusalemu?