21. Lakini Abishai, mwana wa Seruya, akajibu na kusema, Je! Shimei hatauawa kwa sababu hii, kwa kuwa amemlaani masihi wa BWANA?
22. Lakini Daudi akasema, Mimi nina nini nanyi, enyi wana wa Seruya, hata mmekuwa adui zangu leo? Je! Atauawa mtu ye yote leo katika Israeli? Kwa maana sijui mimi leo ya kwamba ndimi mfalme juu ya Israeli?
23. Kisha mfalme akamwambia Shimei, Hutakufa. Mfalme akamwapia.
24. Kisha Mefiboshethi, mwana wa Sauli, akashuka ili amlaki mfalme; alikuwa hakukata kucha za miguu yake wala kukata ndevu zake, wala kufua nguo zake, tangu siku alipoondoka mfalme, hata siku hiyo aliporudi kwake kwa amani.
25. Basi ikawa, alipofika Yerusalemu kumlaki mfalme, mfalme akamwambia, Mbona hukwenda pamoja nami, Mefiboshethi?
26. Naye akajibu, Bwana wangu, Ee mfalme, mtumwa wangu alinidanganya; kwa kuwa mimi mtumwa wako nilisema, Nitajitandikia punda, nipate kumpanda, na kwenda pamoja na mfalme; kwa sababu mimi mtumwa wako ni kiwete.
27. Naye amenisingizia mimi mtumwa wako kwa bwana wangu mfalme; lakini bwana wangu mfalme ni kama malaika wa Mungu; utende basi yaliyo mema machoni pako.