20. mtumwa wako Yoabu ameyatenda haya ili kubadili uso wa jambo hili; na bwana wangu anayo akili, kama akili ya malaika wa Mungu, hata ajue mambo yote ya duniani.
21. Basi mfalme akamwambia Yoabu, Angalia sasa, nimekata shauri hili; nenda, ukamrudishe tena yule kijana Absalomu.
22. Naye Yoabu akaanguka kifulifuli hata nchi, akasujudu, akambariki mfalme, Yoabu akasema, Leo mimi mtumwa wako najua ya kwamba nimepata neema machoni pako, bwana wangu mfalme, kwa kuwa mfalme amemfanyia mtumwa wake haja yake.
23. Basi Yoabu akaondoka, akaenda Geshuri, akamleta Absalomu Yerusalemu.
24. Naye mfalme akasema, Ageukie nyumbani kwake, asinione uso wangu. Basi Absalomu akarejea nyumbani kwake, asimwone uso mfalme.
25. Basi katika Israeli wote hapakuwa na mtu hata mmoja mwenye kusifiwa kwa uzuri wake kama huyo Absalomu; tangu nyayo za miguu yake hata utosi wa kichwa chake hapakuwa na ila kwake.
26. Naye aliponyoa kichwa, (basi mwisho wa kila mwaka hunyoa; na kwa sababu nywele zilikuwa nzito kwake, kwa hiyo akanyoa;) hupima nywele za kichwa chake shekeli mia mbili kwa uzani wa mfalme.
27. Kisha wakazaliwa kwake Absalomu wana watatu na binti mmoja, ambaye jina lake aliitwa Tamari; naye alikuwa mwanamke mzuri wa uso.
28. Absalomu akakaa miaka miwili mizima katika Yerusalemu; asimwone uso mfalme.
29. Ndipo Absalomu akatuma kumwita Yoabu, ampeleke kwa mfalme, lakini yeye akakataa kumjia; akatuma tena mara ya pili, lakini akakataa kuja.