13. Mwanamke akasema, Kwa nini basi wewe umewafikiria mambo kama hayo watu wa Mungu? Kwani kwa kunena neno hili mfalme ni kama mwenye hatia, kwa kuwa mfalme hamleti kwao tena yule mfukuzwa wake.
14. Kwa kuwa hatuna budi kufa, nasi tu kama maji yaliyomwagika chini, yasiyowezekana kuzoleka tena; wala Mungu haondoi maisha ila hufikiri shauri, kwamba yeye aliyefukuzwa asiwe mkimbizi kwake.
15. Hata sasa nilivyokuja mimi kunena neno hili na bwana wangu mfalme, ni kwa sababu watu wamenitisha; nami, mjakazi wako, nikasema, Mimi nitanena sasa kwa mfalme; labda itakuwa mfalme atanifanyia haja yangu mimi mtumwa wake.
16. Kwa kuwa mfalme atasikia, ili amwokoe mtumwa wake mkononi mwa yule mtu atakaye kuniharibu mimi na mwanangu pia katika urithi wa Mungu.
17. Ndipo mimi mjakazi wako nikasema, Neno la bwana wangu mfalme na liwe la kustarehesha; kwa kuwa kama malaika wa Mungu ndivyo alivyo bwana wangu mfalme, kuyapambanua yaliyo mema na yaliyo mabaya; naye BWANA, Mungu wako na awe pamoja nawe.
18. Ndipo mfalme akajibu, akamwambia yule mwanamke, usinifiche, nakusihi, neno lo lote nitakalokuuliza. Na mwanamke akasema, Na anene sasa bwana wangu mfalme.
19. Mfalme akasema, Je! Si mkono wa Yoabu ulio pamoja nawe katika haya yote? Mwanamke akajibu, akasema, Kama iishivyo roho yako, bwana wangu, mfalme, hapana mtu awezaye kugeuka kwa kuume, au kwa kushoto, kukana neno lo lote alilolisema bwana wangu mfalme; kwani mtumwa wako Yoabu ndiye aliyeniamuru, na kuyaweka maneno haya yote kinywani mwa mjakazi wako;
20. mtumwa wako Yoabu ameyatenda haya ili kubadili uso wa jambo hili; na bwana wangu anayo akili, kama akili ya malaika wa Mungu, hata ajue mambo yote ya duniani.
21. Basi mfalme akamwambia Yoabu, Angalia sasa, nimekata shauri hili; nenda, ukamrudishe tena yule kijana Absalomu.
22. Naye Yoabu akaanguka kifulifuli hata nchi, akasujudu, akambariki mfalme, Yoabu akasema, Leo mimi mtumwa wako najua ya kwamba nimepata neema machoni pako, bwana wangu mfalme, kwa kuwa mfalme amemfanyia mtumwa wake haja yake.
23. Basi Yoabu akaondoka, akaenda Geshuri, akamleta Absalomu Yerusalemu.
24. Naye mfalme akasema, Ageukie nyumbani kwake, asinione uso wangu. Basi Absalomu akarejea nyumbani kwake, asimwone uso mfalme.