1. Basi Yoabu, mwana wa Seruya, akatambua ya kuwa moyo wa mfalme unamwelekea Absalomu.
2. Yoabu akatuma watu waende Tekoa, akaleta kutoka huko mwanamke mwenye akili, akamwambia, Nakusihi, ujifanye kama unakaa matanga, ukavae nguo za kufiwa, nakusihi, wala usijitie mafuta, ila ukafanane na mwanamke aliyeomboleza siku nyingi kwa ajili yake aliyefariki;
3. kisha uingie kwa mfalme ukamwambie maneno haya. Hivyo Yoabu akamtia maneno kinywani.
4. Naye yule mwanamke wa Tekoa aliponena na mfalme, akaanguka kifulifuli chini, akamsujudia, akasema, Nisaidie, Ee mfalme.
5. Mfalme akamwuliza, Una nini? Naye akajibu, Hakika ni mjane mimi, niliyefiwa na mume wangu.
6. Nami mjakazi wako nalikuwa na wana wawili, na hao wawili wakashindana uwandani, wala hapakuwa na mtu wa kuwaamua, lakini mmoja akampiga mwenzake, akamwua.
7. Na tazama, jamaa yote wameniinukia mimi mjakazi wako, wakasema, Mtoe yule aliyempiga nduguye, ili tupate kumwua yeye kwa maisha ya nduguye aliyemwua, hata na kumfisha mrithi pia; ndivyo watakavyolizima kaa langu lililobaki, wasimwachie mume wangu jina wala masalio usoni pa nchi.
8. Mfalme akamwambia huyo mwanamke, Nenda nyumbani kwako, nami nitakufanyia agizo.
9. Ndipo huyo mwanamke wa Tekoa akamwambia mfalme, Na uwe juu yangu, Ee bwana wangu mfalme, na juu ya nyumba ya baba yangu uovu huu; wala kwa mfalme na kwa kiti chake cha enzi pasiwepo hatia.
10. Mfalme akasema, Ye yote atakaye kuambia neno, mlete kwangu, naye hatakugusa tena.
11. Ndipo akajibu, Nakusihi, mfalme na amkumbuke BWANA, Mungu wako, ili mlipiza kisasi cha damu asizidi kuharibu, wasije kumharibu mwanangu. Naye akasema, Aishivyo BWANA, hautaanguka chini hata unywele mmoja wa mwanao.
12. Mwanamke akasema, Mwache mjakazi wako, nakusihi, niseme neno moja kwa bwana wangu mfalme. Akasema, Haya nena.
13. Mwanamke akasema, Kwa nini basi wewe umewafikiria mambo kama hayo watu wa Mungu? Kwani kwa kunena neno hili mfalme ni kama mwenye hatia, kwa kuwa mfalme hamleti kwao tena yule mfukuzwa wake.