20. Huyo Absalomu nduguye akamwambia, je! Amekuwa nawe Amnoni nduguyo? Ila sasa tulia, dada; ni nduguyo; usilitie moyoni jambo hili. Basi Tamari akakaa hali ya ukiwa nyumbani mwa nduguye Absalomu.
21. Na mfalme Daudi alipoyasikia maneno hayo yote, alikasirika sana.
22. Ila Absalomu hakusema na Amnoni wala kwa heri wala kwa shari; kwa maana Absalomu alimchukia Amnoni kwa kumtenza nguvu umbu lake Tamari.
23. Ikawa baada ya miaka miwili mizima, Absalomu alikuwa na wenye kukata manyoya ya kondoo huko Baal-hasori uliopo upande wa Efraimu; naye Absalomu akawaalika wana wote wa mfalme.