5. Akamwambia mfalme, Ndizo kweli habari zile nilizozisikia katika nchi yangu za mambo yako na za hekima yako.
6. Lakini mimi sikuyasadiki maneno yao, hata nilipokuja na kuona kwa macho yangu; wala, tazama, ukuu wa hekima yako sikuambiwa nusu; wewe umezidi kuliko habari nilizozisikia.
7. Heri watu wako, na heri hawa watumishi wako, wasimamao mbele yako sikuzote, wakisikia hekima yako.
8. Na ahimidiwe BWANA, Mungu wako, aliyependezwa nawe, ili akuweke juu ya kiti chake cha enzi, kuwa mfalme wake BWANA, Mungu wako; kwa kuwa Mungu wako amewapenda Israeli, kuwathibitisha milele, kwa hiyo amekufanya kuwa mfalme juu yao, ufanye hukumu na haki.
9. Basi akampa mfalme talanta mia na ishirini za dhahabu, na manukato mengi mengi sana, na vito vya thamani; wala haukuja wingi wa manukato, kama hayo aliyopewa mfalme Sulemani na malkia wa Sheba.
10. Tena watumishi wa Hiramu, pamoja na watumishi wa Sulemani, walioleta dhahabu kutoka Ofiri, wakaleta miti ya msandali, na vito vya thamani.
11. Mfalme akayafanya kwa miti hiyo ya msandali madari ya nyumba ya BWANA, na nyumba ya mfalme, na vinubi na vinanda vya hao waimbaji; wala haijatokea kama hiyo katika nchi ya Yuda.
12. Mfalme Sulemani akampa malkia wa Sheba haja yake yote, kila alilotaka, zaidi ya vile alivyomletea mfalme. Basi akarudi, akaenda zake katika nchi yake, yeye na watumishi wake.
13. Basi uzani wa dhahabu iliyomfikia Sulemani mwaka mmoja, ndio talanta mia sita sitini na sita za dhahabu;
14. mbali na ile waliyoileta wachuuzi na wafanya biashara; tena wafalme wote wa Arabuni, na maliwali wa nchi wakamletea Sulemani dhahabu na fedha.
15. Mfalme Sulemani akafanya ngao mia mbili za dhahabu iliyofuliwa; ngao moja hupata shekeli mia sita za dhahabu iliyofuliwa.
16. Na vigao mia tatu vya dhahabu iliyofuliwa; kigao kimoja hupata shekeli mia tatu za dhahabu; mfalme akaviweka katika nyumba ya mwitu wa Lebanoni.
17. Tena mfalme akafanya kiti cha enzi kikubwa cha pembe, akakifunikiza kwa dhahabu iliyo safi.
18. Kiti kile kilikuwa na daraja sita, tena na kikao cha miguu cha dhahabu, navyo vilikuwa vimeshikamana na kiti; na mikono huko na huko mahali pa kuketi, na simba wawili wakisimama kando ya hiyo mikono.
19. Na simba kumi na wawili wamesimama juu ya daraja sita, huko na huko; wala hakikufanyika kwa mfano wake katika ufalme wo wote.
20. Na vyombo vyote vya kunywea vya mfalme Sulemani vilikuwa vya dhahabu, na vyombo vyote vya nyumba ya mwitu wa Lebanoni vilikuwa vya dhahabu iliyosafika; fedha haikuhesabiwa kuwa kitu siku za Sulemani.