3. Naye malkia wa Sheba alipoona hekima ya Sulemani, na nyumba aliyoijenga,
4. na vyakula vya mezani mwake, na kikao cha watumishi wake, na usimamizi wao wangoje wake, na mavazi yao; na wanyweshaji wake, na mavazi yao; na daraja yake ya kupandia mpaka nyumba ya BWANA; roho yake ilizimia.
5. Akamwambia mfalme, Ndizo kweli habari zile nilizozisikia katika nchi yangu za mambo yako na za hekima yako.
6. Lakini mimi sikuyasadiki maneno yao, hata nilipokuja na kuona kwa macho yangu; wala, tazama, ukuu wa hekima yako sikuambiwa nusu; wewe umezidi kuliko habari nilizozisikia.
7. Heri watu wako, na heri hawa watumishi wako, wasimamao mbele yako sikuzote, wakisikia hekima yako.
8. Na ahimidiwe BWANA, Mungu wako, aliyependezwa nawe, ili akuweke juu ya kiti chake cha enzi, kuwa mfalme wake BWANA, Mungu wako; kwa kuwa Mungu wako amewapenda Israeli, kuwathibitisha milele, kwa hiyo amekufanya kuwa mfalme juu yao, ufanye hukumu na haki.
9. Basi akampa mfalme talanta mia na ishirini za dhahabu, na manukato mengi mengi sana, na vito vya thamani; wala haukuja wingi wa manukato, kama hayo aliyopewa mfalme Sulemani na malkia wa Sheba.
10. Tena watumishi wa Hiramu, pamoja na watumishi wa Sulemani, walioleta dhahabu kutoka Ofiri, wakaleta miti ya msandali, na vito vya thamani.
11. Mfalme akayafanya kwa miti hiyo ya msandali madari ya nyumba ya BWANA, na nyumba ya mfalme, na vinubi na vinanda vya hao waimbaji; wala haijatokea kama hiyo katika nchi ya Yuda.
12. Mfalme Sulemani akampa malkia wa Sheba haja yake yote, kila alilotaka, zaidi ya vile alivyomletea mfalme. Basi akarudi, akaenda zake katika nchi yake, yeye na watumishi wake.
13. Basi uzani wa dhahabu iliyomfikia Sulemani mwaka mmoja, ndio talanta mia sita sitini na sita za dhahabu;
14. mbali na ile waliyoileta wachuuzi na wafanya biashara; tena wafalme wote wa Arabuni, na maliwali wa nchi wakamletea Sulemani dhahabu na fedha.