1. Ikawa miaka ishirini ilipopita, ambayo katika hiyo Sulemani aliijenga nyumba ya BWANA, na nyumba yake mwenyewe;
2. ndipo Sulemani akaijenga miji ile Hiramu aliyompa Sulemani, akawakalisha humo wana wa Israeli.
3. Naye Sulemani akaenda Hamath-zoba, akaushinda.
4. Akaujenga Tadmori wa nyikani, na miji yote ya hazina, aliyoijenga katika Hamathi.
5. Tena akaujenga Beth-horoni wa juu, na Beth-horoni wa chini, miji yenye boma, yenye kuta, na malango, na makomeo;
6. na Baalathi, na miji yote ya hazina Sulemani aliyokuwa nayo, na miji yote ya magari yake, na miji ya wapanda farasi wake, na ya anasa yote aliyopenda Sulemani kujenga humo Yerusalemu, na katika Lebanoni, na katika nchi yote ya mamlaka yake.
7. Basi kwa habari ya watu wote waliosalia wa Wahiti, na wa Waamori, na wa Waperizi, na wa Wahivi, na wa Wayebusi, wasiokuwa wa Israeli;
8. wa watoto wao waliosalia baada yao katika nchi, ambao wana wa Israeli hawakuwakomesha, katika hao Sulemani akawatumikisha shokoa hata leo.
9. Wala katika wana wa Israeli Sulemani hakuwafanya watumwa kazini mwake; lakini hao walikuwa watu wa vita, na wakuu wa majemadari wake, na maakida wa magari yake na wa wapanda farasi wake.
10. Na hao walikuwa maakida wakuu wa Sulemani, watu mia mbili na hamsini, waliotawala juu ya watu.
11. Sulemani akamleta binti Farao kutoka mji wa Daudi mpaka nyumba aliyomjengea; kwa kuwa alisema, Mke wangu hatakaa nyumbani mwa Daudi mfalme wa Israeli, kwa kuwa ni patakatifu, mahali palipofika sanduku la BWANA.