2 Nya. 36:8-17 Swahili Union Version (SUV)

8. Basi mambo yote ya Yehoyakimu yaliyosalia, na machukizo yake aliyoyafanya, nayo yaliyoonekana kwake, tazama, yameandikwa katika kitabu cha wafalme wa Israeli na Yuda; na Yekonia mwanawe akatawala mahali pake.

9. Yekonia alikuwa na umri wa miaka kumi na minane alipoanza kutawala; akatawala katika Yerusalemu miezi mitatu na siku kumi; akafanya yaliyo mabaya machoni pa BWANA.

10. Mwaka ulipokwisha, Nebukadreza akatuma wajumbe, akamchukua mpaka Babeli; pamoja na vyombo vya thamani vya nyumba ya BWANA; akamtawaza Sedekia nduguye awe mfalme juu ya Yuda na Yerusalemu.

11. Sedekia alikuwa na umri wa miaka ishirini na mmoja, alipoanza kutawala; akatawala katika Yerusalemu miaka kumi na mmoja;

12. akafanya yaliyo mabaya machoni pa BWANA, Mungu wake; wala hakujinyenyekesha mbele ya Yeremia nabii aliponena kwa kinywa cha BWANA.

13. Tena akamwasi mfalme Nebukadreza, aliyemwapisha kwa Mungu; lakini akajifanyia shingo ngumu, akajitia moyo nguvu asimgeukie BWANA, Mungu wa Israeli.

14. Na zaidi ya hayo wakuu wote wa makuhani, na watu, wakakosa mno sawasawa na machukizo yote ya mataifa; wakainajisi nyumba ya BWANA aliyoitakasa katika Yerusalemu.

15. Naye BWANA, Mungu wa baba zao, akatuma kwao kwa mikono ya wajumbe wake, akiondoka mapema, na kutuma; kwa sababu aliwahurumia watu wake, na makao yake;

16. lakini waliwadhihaki wajumbe wa Mungu, na kuyadharau maneno yake, na kuwacheka manabii wake, hata ilipozidi ghadhabu ya BWANA juu ya watu wake, hata kusiwe na kuponya.

17. Kwa hiyo akaleta juu yao mfalme wa Wakaldayo, aliyewaua vijana wao kwa upanga nyumbani mwa patakatifu pao, asiwahurumie kijana wala mwanamwali, mzee wala mkongwe; akawatia wote mkononi mwake.

2 Nya. 36