2 Nya. 33:6-18 Swahili Union Version (SUV)

6. Tena akawapitisha wanawe motoni katika bonde la mwana wa Hinomu; akatazama bao, akabashiri, akafanya uganga, akajishughulisha na hao wenye pepo wa utambuzi, na wachawi; akafanya mabaya mengi machoni pa BWANA, hata kumkasirisha.

7. Akaiweka sanamu ya kuchonga aliyoifanya, katika nyumba ya Mungu ambayo Mungu alimwambia Daudi, na Sulemani mwanawe, Katika nyumba hii, na katika Yerusalemu, niliouchagua miongoni mwa kabila zote za Israeli, nitaliweka jina langu milele;

8. wala sitawaondoshea miguu tena Israeli katika nchi niliyowaagizia baba zenu; wakiangalia tu kutenda yote niliyowaamuru, yaani, torati yote, na sheria, na maagizo, niliyowaamuru kwa mkono wa Musa.

9. Basi Manase akawakosesha Yuda na wenyeji wa Yerusalemu, hata wakazidi kufanya mabaya kuliko mataifa, aliowaharibu BWANA mbele ya wana wa Israeli.

10. Naye BWANA akasema na Manase, na watu wake; wala wasiangalie.

11. Kwa hiyo BWANA akaleta juu yao maakida wa jeshi la mfalme wa Ashuru, waliomkamata Manase kwa minyororo, wakamfunga kwa pingu, wakamchukua mpaka Babeli.

12. Hata alipokuwa katika taabu, akamsihi BWANA, Mungu wake, akajinyenyekeza sana mbele za Mungu wa baba zake.

13. Akamwomba; naye akamtakabali, akayasikia maombi yake; akamrudisha tena Yerusalemu katika ufalme wake. Ndipo Manase akajua ya kwamba BWANA ndiye Mungu.

14. Hata baada ya hayo akaujengea mji wa Daudi ukuta wa nje, upande wa magharibi wa Gihoni, bondeni, hata kufika maingilio ya lango la samaki; akauzungusha Ofeli, akauinua juu sana; akaweka maakida mashujaa katika miji yote ya Yuda yenye maboma.

15. Akaiondoa miungu migeni, na hiyo sanamu nyumbani mwa BWANA, na madhabahu zote alizozijenga katika mlima wa nyumba ya BWANA, na Yerusalemu, akazitupa nje ya mji.

16. Akaijenga madhabahu ya BWANA, akatoa juu yake dhabihu za sadaka za amani, na za shukrani, akawaamuru Yuda wamtumikie BWANA, Mungu wa Israeli.

17. Lakini watu wakaendelea kutoa dhabihu katika mahali pa juu, ila wakamtolea BWANA, Mungu wao tu.

18. Basi mambo yote ya Manase yaliyosalia, na maombi yake kwa Mungu wake, na maneno ya waonaji walionena naye kwa jina la BWANA, Mungu wa Israeli, tazama, yameandikwa kati ya mambo ya wafalme wa Israeli.

2 Nya. 33