13. Akamwomba; naye akamtakabali, akayasikia maombi yake; akamrudisha tena Yerusalemu katika ufalme wake. Ndipo Manase akajua ya kwamba BWANA ndiye Mungu.
14. Hata baada ya hayo akaujengea mji wa Daudi ukuta wa nje, upande wa magharibi wa Gihoni, bondeni, hata kufika maingilio ya lango la samaki; akauzungusha Ofeli, akauinua juu sana; akaweka maakida mashujaa katika miji yote ya Yuda yenye maboma.
15. Akaiondoa miungu migeni, na hiyo sanamu nyumbani mwa BWANA, na madhabahu zote alizozijenga katika mlima wa nyumba ya BWANA, na Yerusalemu, akazitupa nje ya mji.
16. Akaijenga madhabahu ya BWANA, akatoa juu yake dhabihu za sadaka za amani, na za shukrani, akawaamuru Yuda wamtumikie BWANA, Mungu wa Israeli.
17. Lakini watu wakaendelea kutoa dhabihu katika mahali pa juu, ila wakamtolea BWANA, Mungu wao tu.
18. Basi mambo yote ya Manase yaliyosalia, na maombi yake kwa Mungu wake, na maneno ya waonaji walionena naye kwa jina la BWANA, Mungu wa Israeli, tazama, yameandikwa kati ya mambo ya wafalme wa Israeli.
19. Sala yake pia, na jinsi Mungu alivyomtakabali, na dhambi yake yote, na kosa lake, na mahali alipopajenga mahali pa juu, na kupasimamishia maashera na sanamu za kuchonga, kabla ya kujinyenyekeza; tazama, hayo yameandikwa katika tarehe ya Hozai.
20. Basi Manase akalala na babaze, wakamzika nyumbani mwake; na Amoni mwanawe akatawala mahali pake.
21. Amoni alikuwa na umri wa miaka ishirini na miwili alipoanza kutawala; akatawala katika Yerusalemu miaka miwili.
22. Akafanya yaliyo maovu machoni pa BWANA, kama alivyofanya Manase babaye; Amoni akazitolea dhabihu sanamu zote alizozifanya Manase babaye, akazitumikia.
23. Wala hakujinyenyekeza mbele za BWANA, kama Manase babaye alivyojinyenyekeza; lakini huyo Amoni akaongeza makosa juu ya makosa.
24. Wakamfanyia fitina watumishi wake, wakamwua katika nyumba yake mwenyewe.
25. Lakini watu wa nchi wakawaua wote waliomfanyia fitina mfalme Amoni; watu wa nchi wakamfanya Yosia mwanawe awe mfalme badala yake.