5. Akapiga moyo konde, akaujenga ukuta wote uliobomoka, akauinua sawa na minara, na ukuta wa pili nje, akaongeza nguvu ya Milo, katika mji wa Daudi, akafanya silaha na ngao tele.
6. Akaweka maakida wa vita juu ya watu, akawakusanya kwake uwandani penye lango la mji, akawafurahisha mioyo; akisema,
7. Iweni hodari, na wa moyo mkuu, msiogope, wala msifadhaike kwa sababu ya mfalme wa Ashuru, wala kwa majeshi yote walio pamoja naye; kwa maana yupo mkuu pamoja nasi kuliko aliye pamoja naye;
8. kwake upo mkono wa mwili; ila kwetu yupo BWANA, Mungu wetu, kutusaidia, na kutupigania mapigano yetu. Na watu wakayategemea maneno ya Hezekia, mfalme wa Yuda.
9. Na baada ya hayo Senakeribu mfalme wa Ashuru, akatuma watumishi wake waende Yerusalemu, (naye alikuwapo mbele ya Lakishi, na uwezo wake wote pamoja naye,) kwa Hezekia, mfalme wa Yuda, na kwa Yuda wote waliokuwako Yerusalemu, kusema,
10. Senakeribu, mfalme wa Ashuru, asema hivi, Mwatumainia nini hata mkae mkihusuriwa katika Yerusalemu?
11. Siye Hezekia anayewashawishi, mtolewe kufa kwa njaa na kwa kiu, akisema, BWANA, Mungu wetu, atatuokoa na mkono wa mfalme wa Ashuru?
12. Si yeye Hezekia huyo aliyeondoa mahali pake pa juu, na madhabahu zake, akawaamuru Yuda na Yerusalemu, akisema, Abuduni mbele ya madhabahu moja, na juu yake mtafukiza uvumba?
13. Je! Ninyi hamjui mimi na baba zangu tuliyowafanyia watu wote wa nchi? Je! Miungu ya mataifa wa nchi iliweza kuokoa kwa lo lote nchi zao na mkono wangu?
14. Ni yupi miongoni mwa miungu ya mataifa wale walioharibiwa kabisa na baba zangu, aliyeweza kuwaokoa watu wake na mkono wangu, hata Mungu wenu aweze kuwaokoa ninyi na mkono wangu?
15. Basi sasa asiwadanganye Hezekia, wala asiwashawishi kwa hayo, wala msimwamini; kwa kuwa hapana mungu wa taifa lo lote, wala wa ufalme wo wote, aliyeweza kuwaokoa watu wake na mkono wangu, au na mkono wa baba zangu; sembuse Mungu wenu atawaokoaje ninyi na mkono wangu?
16. Na watumishi wake wakazidi kusema juu ya BWANA Mungu, na juu ya Hezekia, mtumishi wake.
17. Tena akaandika waraka, kumtukana BWANA, Mungu wa Israeli, na kumwambia, akisema, Kama vile miungu ya mataifa wa nchi isivyowaokoa watu wao na mkono wangu, vivyo hivyo Mungu wa Hezekia hatawaokoa watu wake na mkono wangu.
18. Wakawalilia kwa sauti kuu, kwa lugha ya Kiyahudi, watu wa Yerusalemu waliokuwako ukutani ili kuwaogofisha, na kuwafadhaisha; hata wapate kuutwaa mji.
19. Wakamnenea Mungu wa Yerusalemu, kana kwamba kuitaja miungu ya mataifa wa nchi, iliyo kazi ya mikono ya watu.
20. Na kwa ajili ya hayo Hezekia mfalme, na Isaya nabii, mwana wa Amozi, wakaomba, wakalia hata mbinguni.
21. Naye BWANA akatuma malaika aliyewakatia mbali mashujaa wote, na majemadari, na maakida, matuoni mwa mfalme wa Ashuru. Basi akarudia nchi yake mwenye haya ya uso. Naye alipoingia nyumbani mwa mungu wake, wale waliotoka viunoni mwake mwenyewe wakamwangamiza humo kwa upanga.
22. Ndivyo BWANA alivyomwokoa Hezekia, na wenyeji wa Yerusalemu, na mkono wa Senakeribu, mfalme wa Ashuru, na mikononi mwa wote, akawaongoza pande zote.
23. Watu wengi walimletea BWANA zawadi huko Yerusalemu, na vitu vya thamani kwa Hezekia, mfalme wa Yuda; hata yeye akatukuka tangu wakati ule machoni pa mataifa yote.
24. Katika siku hizo Hezekia akaugua akawa katika hatari ya kufa; akamwomba BWANA; naye akasema naye, akampa ishara.