2. Basi Hezekia, alipoona ya kuwa Senakeribu amekuja, na kuazimia kupigana na Yerusalemu,
3. akafanya shauri na wakuu wake, na mashujaa wake, kuzuia maji ya chemchemi zilizokuwa nje ya mji; nao wakamsaidia.
4. Wakakusanyika watu wengi, wakazizuia chemchemi zote, na kijito kilichopita kati ya nchi, wakisema, Kwa nini, wakifika wafalme wa Ashuru, waone maji mengi?
5. Akapiga moyo konde, akaujenga ukuta wote uliobomoka, akauinua sawa na minara, na ukuta wa pili nje, akaongeza nguvu ya Milo, katika mji wa Daudi, akafanya silaha na ngao tele.
6. Akaweka maakida wa vita juu ya watu, akawakusanya kwake uwandani penye lango la mji, akawafurahisha mioyo; akisema,
7. Iweni hodari, na wa moyo mkuu, msiogope, wala msifadhaike kwa sababu ya mfalme wa Ashuru, wala kwa majeshi yote walio pamoja naye; kwa maana yupo mkuu pamoja nasi kuliko aliye pamoja naye;
8. kwake upo mkono wa mwili; ila kwetu yupo BWANA, Mungu wetu, kutusaidia, na kutupigania mapigano yetu. Na watu wakayategemea maneno ya Hezekia, mfalme wa Yuda.
9. Na baada ya hayo Senakeribu mfalme wa Ashuru, akatuma watumishi wake waende Yerusalemu, (naye alikuwapo mbele ya Lakishi, na uwezo wake wote pamoja naye,) kwa Hezekia, mfalme wa Yuda, na kwa Yuda wote waliokuwako Yerusalemu, kusema,
10. Senakeribu, mfalme wa Ashuru, asema hivi, Mwatumainia nini hata mkae mkihusuriwa katika Yerusalemu?
11. Siye Hezekia anayewashawishi, mtolewe kufa kwa njaa na kwa kiu, akisema, BWANA, Mungu wetu, atatuokoa na mkono wa mfalme wa Ashuru?
12. Si yeye Hezekia huyo aliyeondoa mahali pake pa juu, na madhabahu zake, akawaamuru Yuda na Yerusalemu, akisema, Abuduni mbele ya madhabahu moja, na juu yake mtafukiza uvumba?
13. Je! Ninyi hamjui mimi na baba zangu tuliyowafanyia watu wote wa nchi? Je! Miungu ya mataifa wa nchi iliweza kuokoa kwa lo lote nchi zao na mkono wangu?
14. Ni yupi miongoni mwa miungu ya mataifa wale walioharibiwa kabisa na baba zangu, aliyeweza kuwaokoa watu wake na mkono wangu, hata Mungu wenu aweze kuwaokoa ninyi na mkono wangu?