1. Hezekia akatuma wajumbe kwa Israeli wote na Yuda pia; akawaandikia nyaraka Efraimu na Manase, waje nyumbani kwa BWANA Yerusalemu, ili wamfanyie pasaka BWANA, Mungu wa Israeli.
2. Kwa maana mfalme na wakuu wake, na kusanyiko lote katika Yerusalemu walifanya shauri kufanya pasaka mwezi wa pili.
3. Kwa sababu hawakuweza kuifanya wakati ule, kwa kuwa makuhani walikuwa hawajajitakasa wa kutosha, wala watu hawajakusanyika huko Yerusalemu.
4. Likawa neno jema machoni pa mfalme, na kusanyiko lote.
5. Basi wakafanya amri kupiga mbiu kati ya Israeli yote, toka Beer-sheba mpaka Dani, ya kwamba watu waje wamfanyie pasaka BWANA, Mungu wa Israeli, huko Yerusalemu; maana tangu siku nyingi hawakuifanya kama vile ilivyoandikwa.