19. Tena vyombo vyote alivyovitupa mfalme Ahazi alipotawala, hapo alipoasi, tumevitengeza na kuvitakasa; navyo, tazama, vipo mbele ya madhabahu ya BWANA.
20. Ndipo Hezekia mfalme akaamka mapema, akakusanya wakuu wa mji, akapanda nyumbani kwa BWANA.
21. Wakaleta ng’ombe waume saba, na kondoo waume saba, na wana-kondoo saba, na mabeberu saba, kuwa sadaka ya dhambi kwa ajili ya ufalme, na kwa ajili ya patakatifu, na kwa ajili ya Yuda. Akaamuru makuhani, wana wa Haruni, wawatoe madhabahuni pa BWANA.
22. Basi wakawachinja ng’ombe, na makuhani wakaipokea damu, wakainyunyiza madhabahuni; wakawachinja kondoo waume, na kuinyunyiza damu madhabahuni; wakawachinja na wana-kondoo, na kuinyunyiza damu madhabahuni.
23. Wakawaleta karibu mabeberu wa sadaka ya dhambi mbele ya mfalme na kusanyiko; wakawawekea mikono yao;
24. na makuhani wakawachinja, wakaitoa damu yao kuwa sadaka ya dhambi madhabahuni, ili kuwafanyia Israeli wote upatanisho; maana mfalme aliamuru Israeli wote wafanyiwe sadaka ya kuteketezwa na sadaka ya dhambi.