13. na wa wana wa Elisafani, Shimri na Yeueli; na wa wana wa Asafu, Zekaria na Matania;
14. na wa wana wa Hemani, Yehueli na Shimei; na wa wana wa Yeduthuni, Shemaya na Uzieli.
15. Wakawakusanya ndugu zao, wakajitakasa, wakaingia, kama alivyoamuru mfalme kwa maneno ya BWANA, ili waisafishe nyumba ya BWANA.
16. Nao makuhani wakaingia nyumbani mwa BWANA, katika mahali pa ndani, ili waisafishe, wakatoa uchafu wote waliouona hekaluni mwa BWANA, wakautupa nje uani mwa nyumba ya BWANA. Walawi wakautwaa, ili wauchukue nje mpaka kijito cha Kidroni.
17. Basi wakaanza kutakasa siku ya kwanza ya mwezi wa kwanza, hata siku ya nane ya mwezi wakafika katika ukumbi wa BWANA; wakaitakasa nyumba ya BWANA katika muda wa siku nane; wakamaliza siku ya kumi na sita ya mwezi wa kwanza.
18. Wakaingia ndani kwa Hezekia mfalme, wakasema, Tumeisafisha nyumba yote ya BWANA, na madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa, pamoja na vyombo vyake vyote, na meza ya mikate ya wonyesho, pamoja na vyombo vyake vyote.
19. Tena vyombo vyote alivyovitupa mfalme Ahazi alipotawala, hapo alipoasi, tumevitengeza na kuvitakasa; navyo, tazama, vipo mbele ya madhabahu ya BWANA.
20. Ndipo Hezekia mfalme akaamka mapema, akakusanya wakuu wa mji, akapanda nyumbani kwa BWANA.
21. Wakaleta ng’ombe waume saba, na kondoo waume saba, na wana-kondoo saba, na mabeberu saba, kuwa sadaka ya dhambi kwa ajili ya ufalme, na kwa ajili ya patakatifu, na kwa ajili ya Yuda. Akaamuru makuhani, wana wa Haruni, wawatoe madhabahuni pa BWANA.
22. Basi wakawachinja ng’ombe, na makuhani wakaipokea damu, wakainyunyiza madhabahuni; wakawachinja kondoo waume, na kuinyunyiza damu madhabahuni; wakawachinja na wana-kondoo, na kuinyunyiza damu madhabahuni.
23. Wakawaleta karibu mabeberu wa sadaka ya dhambi mbele ya mfalme na kusanyiko; wakawawekea mikono yao;
24. na makuhani wakawachinja, wakaitoa damu yao kuwa sadaka ya dhambi madhabahuni, ili kuwafanyia Israeli wote upatanisho; maana mfalme aliamuru Israeli wote wafanyiwe sadaka ya kuteketezwa na sadaka ya dhambi.
25. Akawasimamisha Walawi nyumbani mwa BWANA wenye matoazi, wenye vinanda, na wenye vinubi, kama alivyoamuru Daudi, na Gadi mwonaji wa mfalme, na Nathani nabii; kwani BWANA aliamuru hivi kwa manabii wake.