1. Ahazi alikuwa na umri wa miaka ishirini alipoanza kutawala; akatawala katika Yerusalemu miaka kumi na sita; wala hakufanya yaliyo ya adili machoni pa BWANA, kama Daudi babaye;
2. bali akaziendea njia za wafalme wa Israeli, akawafanyizia mabaali sanamu za kusubu.
3. Tena akafukiza uvumba katika bonde la mwana wa Hinomu, akawateketeza wanawe motoni, sawasawa na machukizo ya mataifa, aliowafukuza BWANA mbele ya wana wa Israeli.
4. Akatoa dhabihu na kufukiza uvumba katika mahali pa juu, na vilimani, na chini ya kila mti wenye majani mabichi.
5. Kwa hiyo BWANA, Mungu wake, akamtia mkononi mwa mfalme wa Shamu; wakampiga, wakachukua wa watu wake wafungwa wengi sana, wakawaleta Dameski. Tena akatiwa mkononi mwa mfalme wa Israeli, aliyempiga mapigo makuu.