2 Nya. 25:15-26 Swahili Union Version (SUV)

15. Kwa hiyo hasira ya BWANA ikawaka juu ya Amazia, akampelekea nabii, aliyemwambia, Mbona umeitafuta miungu ya watu, isiyowaokoa watu wao mkononi mwako?

16. Ikawa, aliposema naye, mfalme akamwambia, Je! Tumekutia wewe kuwa mshauri wa mfalme? Nyamaza; kwa nini upigwe? Ndipo yule nabii akaacha, akasema, Najua ya kuwa Mungu amekusudia kukuangamiza, kwa sababu umeyafanya haya, wala hukulisikiliza shauri langu.

17. Ndipo mfalme Amazia akafanya shauri, akatuma wajumbe kwa Yehoashi, mwana wa Yehoahazi mwana wa Yehu, mfalme wa Israeli, kusema, Njoo, tutazamane uso kwa uso.

18. Na Yehoashi mfalme wa Israeli akatuma wajumbe kwa Amazia mfalme wa Yuda, kusema, Mbaruti uliokuwako Lebanoni ukatuma kwa mwerezi uliokuwako Lebanoni kusema, Umwoze mwanangu binti yako; kukapita hayawani aliyekuwako Lebanoni, akaukanyaga ule mbaruti.

19. Wasema, Tazama, umewapiga Edomu; na moyo wako wakutukuza ujisifu; kaa nyumbani mwako basi; mbona unataka kujitia bure katika madhara, hata uanguke, wewe na Yuda pamoja nawe?

20. Lakini Amazia hakutaka kusikia, kwa maana hayo yalitoka kwa Mungu, ili awatie mikononi mwao, kwa kuwa wameitafuta miungu ya Edomu.

21. Basi Yehoashi mfalme wa Israeli akakwea; wakatazamana uso kwa uso, yeye na Amazia mfalme wa Yuda huko Beth-shemeshi, ulio wa Yuda.

22. Yuda wakashindwa mbele ya Israeli; wakakimbia kila mtu hemani kwake.

23. Yehoashi mfalme wa Israeli akamtwaa Amazia mfalme wa Yuda, mwana wa Yoashi, mwana wa Ahazia, huko Beth-shemeshi, akamchukua mpaka Yerusalemu, akauvunja ukuta wa Yerusalemu, toka lango la Efraimu mpaka lango la pembeni, mikono mia nne.

24. Akaitwaa dhahabu yote, na fedha, na vyombo vyote vilivyoonekana nyumbani mwa Mungu kwa Obed-edomu, na hazina za nyumba ya mfalme, tena watu kuwa amana, akarudi Samaria.

25. Naye Amazia mwana wa Yoashi mfalme wa Yuda, akaishi baada ya kufa kwake Yehoashi mwana wa Yehoahazi, mfalme wa Israeli, miaka kumi na mitano.

26. Na mambo yote ya Amazia yaliyosalia, ya kwanza na ya mwisho, tazama, je! Hayakuandikwa katika kitabu cha wafalme wa Yuda na Israeli?

2 Nya. 25