2 Nya. 24:15-24 Swahili Union Version (SUV)

15. Lakini Yehoyada akawa mzee, mwenye umri mwingi, akafa; alipokufa alikuwa na umri wa miaka mia na thelathini.

16. Wakamzika katika mji wa Daudi kati ya wafalme, kwa sababu ametenda mema katika Israeli, na kwa Mungu, na katika nyumba yake.

17. Hata baada ya kufa kwake Yehoyada, wakuu wa Yuda wakamwendea mfalme, wakamsujudia. Naye mfalme akawasikiliza maneno yao.

18. Wakaiacha nyumba ya BWANA, Mungu wa baba zao; wakatumikia maashera na sanamu; ghadhabu ikawajia Yuda na Yerusalemu kwa sababu ya hiyo hatia yao.

19. Hata hivyo akawapelekea manabii, ili kuwarudisha kwa BWANA; nao wakawashuhudia; lakini hawakukubali kuwasikiliza.

20. Na roho ya Mungu ikamjia Zekaria, mwana wa Yehoyada, kuhani; naye akasimama juu ya watu, akawaambia, Mungu asema hivi, Kwani ninyi kuzihalifu amri za BWANA, hata msiweze kufanikiwa? Kwa kuwa mmemwacha BWANA, yeye naye amewaacha ninyi.

21. Basi, wakafanya shauri juu yake, wakampiga kwa mawe kwa amri ya mfalme katika ua wa nyumba ya BWANA.

22. Basi hivyo mfalme Yoashi hakuukumbuka wema, ambao Yehoyada, baba yake, alimfanyia, bali alimwua mwanawe. Naye alipokufa, alisema, BWANA na ayaangalie haya, akayatakie kisasi.

23. Ikawa mwisho wa mwaka, wakakwea juu yake jeshi la Washami; wakafika Yuda na Yerusalemu, wakawaangamiza wakuu wa watu wote miongoni mwa watu, wakamletea mfalme wa Dameski nyara zao zote.

24. Maana wakaja jeshi la Washami watu haba; BWANA akatia mikononi mwao jeshi kubwa mno, kwa sababu wamemwacha BWANA, Mungu wa baba zao. Hivyo wakamfanyia Yoashi hukumu.

2 Nya. 24