2 Nya. 16:1-6 Swahili Union Version (SUV)

1. Katika mwaka wa thelathini na sita wa kutawala kwake Asa, Baasha mfalme wa Israeli akapanda juu ya Yuda, akaujenga Rama, ili asimwache mtu ye yote kutoka wala kuingia kwa Asa mfalme wa Yuda.

2. Ndipo Asa akatoa fedha na dhahabu katika hazina za nyumba ya BWANA, na nyumba ya mfalme, akampelekea Ben-hadadi mfalme wa Shamu, aliyekaa Dameski, akasema,

3. Kwangu na kwako na liwe agano kama lilivyokuwa kwa baba yangu na baba yako; angalia, nimekuletea fedha na dhahabu; basi, uvunje agano lako na Baasha, mfalme wa Israeli, ili aniondokee mimi.

4. Naye Ben-hadadi akamsikiliza mfalme Asa, akawapeleka maakida wa majeshi yake juu ya miji ya Israeli; wakapiga Iyoni, na Dani, na Abel-maimu, na miji ya hazina yote ya Naftali.

5. Ikawa Baasha aliposikia habari hiyo, akaacha kuujenga Rama, akaikomesha kazi yake.

6. Ndipo mfalme Asa akawatwaa Yuda wote; nao wakayachukua mawe ya Rama, na miti yake, aliyoijengea Baasha; naye akajenga kwa vitu hivyo Geba na Mispa.

2 Nya. 16