1. Basi Abiya akalala na baba zake, wakamzika mjini mwa Daudi, akatawala Asa mwanawe mahali pake; katika siku zake nchi ikastarehe miaka kumi.
2. Basi, Asa akafanya yaliyo mema, yaliyo ya adili, machoni pa BWANA, Mungu wake;
3. maana aliziondoa madhabahu za kigeni, na mahali pa juu, akazivunja nguzo, akayakata-kata maashera;
4. akawaamuru Yuda wamtafute BWANA, Mungu wa baba zao, na kuzitenda torati na amri.
5. Tena akaondoa kutoka miji yote ya Yuda mahali pa juu na sanamu za jua; ufalme ukastarehe mbele yake.
6. Akajenga miji yenye maboma katika Yuda; kwa kuwa nchi ilikuwa imestarehe, wala hakuwa na vita miaka ile; kwa sababu BWANA amemstarehesha.
7. Naye akawaambia Yuda, Na tuijenge miji hii, na kuizungushia maboma, na minara, na malango, na makomeo; nchi bado ikalipo mbele yetu, kwa kuwa tumemtafuta BWANA, Mungu wetu; naam, tumemtafuta, naye amemstarehesha pande zote. Basi wakajenga, wakafanikiwa.
8. Naye Asa alikuwa na jeshi waliochukua ngao na mikuki, katika Yuda mia tatu elfu; na katika Benyamini wenye kuchukua vigao na kupinda upinde, mia mbili na themanini elfu; hao wote walikuwa mashujaa.
9. Kisha, akatoka juu yao Zera Mkushi, mwenye jeshi elfu elfu, na magari mia tatu; akaja Maresha.
10. Akatoka Asa amlaki, wakapanga vita Maresha bondeni mwa Sefatha.
11. Naye Asa akamlilia BWANA, Mungu wake, akasema, BWANA, hapana kuliko wewe aliye wa kusaidia, kati yake yeye aliye hodari, na yeye asiye na nguvu; utusaidie, Ee BWANA, Mungu wetu; kwa kuwa sisi twakutegemea wewe, na kwa jina lako tumekuja juu ya jamii kubwa hii. Ee BWANA, wewe ndiwe Mungu wetu, asikushinde mwanadamu.