1. Basi Abiya akalala na baba zake, wakamzika mjini mwa Daudi, akatawala Asa mwanawe mahali pake; katika siku zake nchi ikastarehe miaka kumi.
2. Basi, Asa akafanya yaliyo mema, yaliyo ya adili, machoni pa BWANA, Mungu wake;
3. maana aliziondoa madhabahu za kigeni, na mahali pa juu, akazivunja nguzo, akayakata-kata maashera;
4. akawaamuru Yuda wamtafute BWANA, Mungu wa baba zao, na kuzitenda torati na amri.
5. Tena akaondoa kutoka miji yote ya Yuda mahali pa juu na sanamu za jua; ufalme ukastarehe mbele yake.
6. Akajenga miji yenye maboma katika Yuda; kwa kuwa nchi ilikuwa imestarehe, wala hakuwa na vita miaka ile; kwa sababu BWANA amemstarehesha.
7. Naye akawaambia Yuda, Na tuijenge miji hii, na kuizungushia maboma, na minara, na malango, na makomeo; nchi bado ikalipo mbele yetu, kwa kuwa tumemtafuta BWANA, Mungu wetu; naam, tumemtafuta, naye amemstarehesha pande zote. Basi wakajenga, wakafanikiwa.
8. Naye Asa alikuwa na jeshi waliochukua ngao na mikuki, katika Yuda mia tatu elfu; na katika Benyamini wenye kuchukua vigao na kupinda upinde, mia mbili na themanini elfu; hao wote walikuwa mashujaa.
9. Kisha, akatoka juu yao Zera Mkushi, mwenye jeshi elfu elfu, na magari mia tatu; akaja Maresha.
10. Akatoka Asa amlaki, wakapanga vita Maresha bondeni mwa Sefatha.