1. Nasi tukitenda kazi pamoja naye twawasihi msiipokee neema ya Mungu bure.
2. (Kwa maana asema,Wakati uliokubalika nalikusikia,Siku ya wokovu nalikusaidia;tazama, wakati uliokubalika ndio sasa; tazama, siku ya wokovu ndiyo sasa.)
3. Tusiwe kwazo la namna yo yote katika jambo lo lote, ili utumishi wetu usilaumiwe;
4. bali katika kila neno tujipatie sifa njema, kama watumishi wa Mungu; katika saburi nyingi, katika dhiki, katika misiba, katika shida;
5. katika mapigo, katika vifungo, katika fitina, katika taabu, katika kukesha, katika kufunga;
6. katika kuwa safi, katika elimu, katika uvumilivu, katika utu wema, katika Roho Mtakatifu, katika upendo usio unafiki;
7. katika neno la kweli, katika nguvu ya Mungu; kwa silaha za haki za mkono wa kuume na za mkono wa kushoto;
8. kwa utukufu na aibu; kwa kunenwa vibaya na kunenwa vema; kama wadanganyao, bali tu watu wa kweli;
9. kama wasiojulikana, bali wajulikanao sana; kama wanaokufa, kumbe tu hai; kama wanaorudiwa, bali wasiouawa;
10. kama wenye huzuni, bali siku zote tu wenye furaha; kama maskini, bali tukitajirisha wengi; kama wasio na kitu, bali tu wenye vitu vyote.
11. Vinywa vyetu vimefumbuliwa kwenu, enyi Wakorintho; mioyo yetu imekunjuliwa.