6. Lakini nijapokuwa mimi ni mtu asiyejua kunena, hii si hali yangu katika elimu; ila katika kila neno tumedhihirishwa kwenu.
7. Je! Nalifanya dhambi kwa kunyenyekea ili ninyi mtukuzwe, kwa sababu naliwahubiri Injili ya Mungu bila ujira?
8. Naliwanyang’anya makanisa mengine mali yao, nikitwaa posho langu ili niwahudumie ninyi.
9. Nami nilipokuwa pamoja nanyi na kuhitaji sikumlemea mtu. Maana hao ndugu waliokuja kutoka Makedonia walinipa kadiri ya mahitaji yangu; nami katika mambo yote najilinda nafsi yangu nisiwalemee hata kidogo; tena najilinda.
10. Kama vile ile kweli ya Kristo ilivyo ndani yangu, hakuna mtu atakayenifumba kinywa katika kujisifu huku, katika mipaka ya Akaya.
11. Kwa nini? Je! Ni kwa sababu siwapendi ninyi? Mungu anajua.
12. Lakini nifanyalo nitalifanya, ili niwapinge hao watafutao nafasi wasipate nafasi; ili kwamba katika neno hilo wajisifialo waonekane kuwa kama sisi.
13. Maana watu kama hao ni mitume wa uongo, watendao kazi kwa hila, wanaojigeuza wawe mfano wa mitume wa Kristo.
14. Wala si ajabu. Maana Shetani mwenyewe hujigeuza awe mfano wa malaika wa nuru.
15. Basi si neno kubwa watumishi wake nao wakijigeuza wawe mfano wa watumishi wa haki, ambao mwisho wao utakuwa sawasawa na kazi zao.
16. Nasema tena, mtu asidhani ya kuwa mimi ni mpumbavu; lakini mjaponidhania hivi, mnikubali kama mpumbavu; ili mimi nami nipate kujisifu ngaa kidogo.
17. Ninenalo silineni agizo la Bwana, bali kama kwa upumbavu, katika ujasiri huu wa kujisifu.