18. na kuitupa miungu yao motoni; kwa maana haikuwa miungu, bali ni kazi ya mikono ya wanadamu; ilikuwa miti na mawe tu, ndiyo sababu wakaiharibu.
19. Basi sasa, Ee BWANA, Mungu wetu, utuokoe na mkono wake, nakusihi, ili kwamba falme zote za dunia zipate kujua ya kuwa wewe ndiwe BWANA Mungu, wewe peke yako.
20. Ndipo Isaya, mwana wa Amozi, akapeleka ujumbe kwa Hezekia, akisema, BWANA, Mungu wa Israeli, asema hivi, Kwa kuwa umeniomba juu ya Senakeribu, mfalme wa Ashuru, mimi nimekusikia.
21. Tamko alilolitamka BWANA katika habari zake ndilo hili, Bikira, binti Sayuni, amekudharau, na kukudhihaki sana; binti Yerusalemu ametikisa kichwa chake juu yako.
22. Ni nani uliyemshutumu na kumtukana? Umeinua sauti yako juu ya nani, na kuinua macho yako juu? Juu ya Mtakatifu wa Israeli.
23. Kwa vinywa vya wajumbe wako umemshutumu Bwana, ukasema, Kwa wingi wa magari yangu nimepanda juu ya vilele vya milima, mpaka mahali pa ndani pa Lebanoni. Nami nitaikata mierezi yake mirefu, na misunobari yake mizuri; nami nitaingia ndani ya makazi yake yaliyo mbali sana, na msitu wa shamba lake lizaalo sana.
24. Nimechimba na kunywa maji mageni, na kwa nyayo za miguu yangu nitaikausha mito yote ya Misri.
25. Je! Hukusikia wewe ya kuwa mimi ndimi niliyeyatenda hayo tokea zamani, na kuyafanya tokea siku za kale? Sasa mimi nimelitimiza jambo hili, iwe kazi yako kuangamiza miji yenye boma, hata ikawe chungu na magofu.
26. Ndiyo sababu wenyeji wao walikuwa na nguvu chache, wakafadhaika, na kuhangaika; wakawa kama majani ya mashamba, kama miche mibichi, kama majani juu ya dari, na kama ngano iliyokaushwa kabla haijaiva.
27. Lakini nakujua, kuketi kwako, na kutoka kwako, na kuingia kwako; na ghadhabu yako unayonighadhibikia.
28. Kwa sababu ya kunighadhibikia kwako, na kwa sababu kutakabari kwako kumefika masikioni mwangu; kwa sababu hiyo nitatia kulabu yangu puani mwako, na hatamu yangu midomoni mwako, nami nitakurudisha nyuma kwa njia ile ile uliyoijia.
29. Na kwako wewe hii ndiyo dalili; mwaka huu mtakula vitu viotavyo vyenyewe; na mwaka wa pili mtakula mazao ya vitu hivyo; na mwaka wa tatu pandeni mbegu, kavuneni; mkapande mashamba ya mizabibu, mkale matunda yake.
30. Na mabaki yaliyookoka ya nyumba ya Yuda yatatia mizizi chini, na kuzaa matunda juu.
31. Maana mabaki yatatoka katika Yerusalemu, na wao watakaookoka katika mlima wa Sayuni wivu wa BWANA utatimiza jambo hilo.