1. Ikawa katika mwaka wa tatu wa Hoshea, mwana wa Ela, mfalme wa Israeli, Hezekia, mwana wa Ahazi, mfalme wa Yuda, alianza kutawala.
2. Alikuwa na umri wa miaka ishirini na mitano alipoanza kutawala; akatawala miaka ishirini na kenda katika Yerusalemu; na jina la mama yake aliitwa Abiya, binti Zekaria.
3. Akafanya yaliyo mema machoni pa BWANA, mfano wa yote aliyoyafanya Daudi, baba yake.
4. Alipaondoa mahali pa juu, akazibomoa nguzo, akaikata hiyo Ashera; akaivunja vipande vipande ile nyoka ya shaba aliyoifanya Musa; maana hata siku zile wana wa Israeli walikuwa wakiifukizia uvumba; naye akaiita jina lake Nehushtani.
5. Alimtumaini BWANA, Mungu wa Israeli; hata baada yake hapakuwa na mfano wake katika wafalme wote wa Yuda, wala katika hao waliomtangulia.
6. Maana alishikamana na BWANA, hakuacha kumfuata, bali alizishika amri zake BWANA alizomwamuru Musa.