19. Akaja Pulu mfalme wa Ashuru juu ya nchi; naye Menahemu akampa Pulu talanta elfu za fedha, ili kwamba mkono wake uwe pamoja naye, na ufalme uwe imara mkononi mwake.
20. Na Menahemu akawatoza Israeli fedha hiyo, yaani, wakuu wote wenye mali, kila mtu shekeli hamsini za fedha, ili ampe huyo mfalme wa Ashuru. Basi mfalme wa Ashuru akarejea, wala hakukaa huko katika nchi.
21. Basi mambo yote ya Menahemu yaliyosalia, na yote aliyoyafanya, je! Hayakuandikwa katika kitabu-cha-tarehe cha wafalme wa Israeli?
22. Menahemu akalala na babaze; na Pekahia mwanawe akatawala mahali pake.
23. Katika mwaka wa hamsini wa Uzia mfalme wa Yuda Pekahia mwana wa Menahemu alianza kutawala juu ya Israeli hatika Samaria; akatawala miaka miwili.
24. Akafanya yaliyo maovu machoni pa BWANA; hakuyaacha makosa ya Yeroboamu mwana wa Nebati, ambayo kwa hayo aliwakosesha Israeli.
25. Na Peka mwana wa Remalia, jemadari wake, akamfanyia fitina, akampiga huko Samaria, katika ngome ya nyumba ya mfalme, pamoja na Argobu na Arie; na pamoja naye walikuwako watu hamsini wa Wagileadi. Akamwua, akatawala mahali pake.
26. Basi mambo yote ya Pekahia yaliyosalia, na yote aliyoyafanya, tazama, yameandikwa katika kitabu-cha-tarehe cha wafalme wa Israeli.
27. Katika mwaka wa hamsini na mbili wa Uzia mfalme wa Yuda Peka mwana wa Remalia alianza kutawala juu ya Israeli katika Samaria; akatawala miaka ishirini.
28. Akafanya yaliyo maovu machoni pa BWANA; hakuyaacha makosa ya Yeroboamu mwana wa Nebati, ambayo kwa hayo aliwakosesha Israeli.
29. Katika siku za Peka mfalme wa Israeli akaja Tiglath-pileseri mfalme wa Ashuru, akatwaa Iyoni, na Abel-beth-maaka, na Yanoa, na Kedeshi, na Hazori, na Gileadi, na Galilaya, nchi yote ya Naftali; akawahamisha hao watu mpaka Ashuru.
30. Na Hoshea mwana wa Ela akafanya fitina juu ya Peka mwana wa Remalia, akampiga, akamwua, akatawala mahali pake, katika mwaka wa ishirini wa Yothamu mwana wa Uzia.
31. Basi mambo yote ya Peka yaliyosalia, na yote aliyoyafanya, tazama, yameandikwa katika kitabu-cha-tarehe cha wafalme wa Israeli.
32. Katika mwaka wa pili wa Peka mwana wa Remalia mfalme wa Israeli Yothamu mwana wa Uzia mfalme wa Yuda alianza kutawala.
33. Alikuwa na umri wa miaka ishirini na mitano alipoanza kutawala; akatawala miaka kumi na sita katika Yerusalemu; na jina la mamaye aliitwa Yerusha binti Sadoki.
34. Akafanya yaliyo mema machoni pa BWANA; akafanya kama yote aliyoyafanya Uzia baba yake.
35. Ila mahali pa juu hapakuondolewa; watu walikuwa wakitoa sadaka na kufukiza uvumba katika mahali pa juu. Ndiye aliyelijenga lango la juu la nyumba ya BWANA.