11. Akafanya yaliyo maovu machoni pa BWANA; hakuyaacha makosa ya Yeroboamu mwana wa Nebati, ambayo kwa hayo aliwakosesha Israeli; lakini akaendelea katika hayo.
12. Basi mambo yote ya Yehoashi yaliyosalia, na yote aliyoyafanya, na ushujaa wake aliopigania na Amazia mfalme wa Yuda, je! Hayakuandikwa katika kitabu-cha-tarehe cha wafalme wa Israeli?
13. Yehoashi akalala na babaze; na Yeroboamu akakaa katika kiti chake cha enzi; naye Yehoashi akazikwa huko Samaria, pamoja na wafalme wa Israeli.
14. Basi Elisha alikuwa ameshikwa na ugonjwa wake uliomwua; naye Yehoashi mfalme wa Israeli akatelemka amtazame, akamlilia mbele yake, akasema, Baba yangu! Baba yangu! Gari la Israeli na wapanda farasi wake!
15. Elisha akamwambia, Twaa uta na mishale; naye akatwaa uta na mishale.
16. Akamwambia mfalme wa Israeli, Weka mkono wako katika uta; naye akaweka mkono wake juu yake. Elisha akaweka mikono yake juu ya mikono ya mfalme.
17. Akasema, Lifungue dirisha linaloelekea mashariki; akalifungua. Basi Elisha akasema, Piga; akapiga. Akasema, Mshale wa BWANA wa kushinda, naam, mshale wa kushinda Shamu, kwa maana utawapiga Washami katika Afeki hata utakapowaangamiza.