1 Sam. 8:5-18 Swahili Union Version (SUV)

5. wakamwambia, Angalia, wewe umekuwa mzee, na wanao hawaendi katika njia zako; basi, tufanyie mfalme atuamue, mfano wa mataifa yote.

6. Lakini neno hilo likawa baya machoni pa Samweli, waliposema, Tupe mfalme atuamue. Naye Samweli akamwomba BWANA.

7. BWANA akamwambia Samweli, Isikilize sauti ya watu hawa katika kila neno watakalokuambia; kwa maana hawakukukataa wewe, bali wamenikataa mimi, ili nisiwe mfalme juu yao.

8. Kwa kadiri ya matendo yote waliyonitenda tokea siku ile nilipowatoa katika Misri hata leo, kwa kuniacha mimi, na kwa kutumikia miungu mingine, ndivyo wanavyokutenda wewe.

9. Basi sasa, isikilize sauti yao; walakini, uwaonye sana, na kuwaonyesha desturi ya mfalme atakayewamiliki.

10. Naye Samweli akawaambia wale watu waliotaka mfalme maneno yote ya BWANA.

11. Akasema, Mfalme atakayewamiliki ninyi atakuwa na desturi hii; atatwaa wana wenu na kuwaweka kwake, kwa magari yake, na kuwa wapanda farasi wake; nao watapiga mbio mbele ya magari yake.

12. Naye atawaweka kwake kuwa maakida juu ya elfu, na maakida juu ya hamsini; na wengine atawaweka walime shamba lake, na kuvuna mavuno yake, na kufanyiza zana zake za vita, na vyombo vya magari yake.

13. Na binti zenu atawatwaa kuwa wafanyaji wa marhamu, na wapishi, na waokaji.

14. Atatwaa makonde yenu, na mashamba yenu ya mizabibu, na ya mizeituni, yale yaliyo mazuri sana, ili awape watumishi wake.

15. Naye atawatoza ushuru wa mbegu zenu na wa mizabibu yenu, awape maakida wake, na watumishi Wake.

16. Atawatwaa watumishi wenu na wajakazi wenu, na ng’ombe zenu walio wazuri sana, na punda zenu, naye atawatia katika kazi zake mwenyewe.

17. Atawatoza fungu la kumi la makundi yenu; nanyi mtakuwa watumwa wake.

18. Nanyi mtalia siku ile kwa sababu ya mfalme wenu mliyejichagulia; BWANA asiwajibu siku ile.

1 Sam. 8