1 Sam. 6:17-21 Swahili Union Version (SUV)

17. Hii ndiyo hesabu ya yale majipu waliyoyapeleka wale Wafilisti, yawe matoleo ya kosa kwa BWANA; kwa Ashdodi moja, kwa Gaza moja, kwa Ashkeloni moja, kwa Gathi moja, na kwa Ekroni moja;

18. na panya wa dhahabu, kwa idadi ya miji yote ya Wafilisti, milki zao wale mashehe watano, miji yenye maboma na vijiji vya mashamba pia. Nalo lile jiwe kubwa, ambalo juu yake waliliweka sanduku la BWANA, liko hata hivi leo hapo kondeni pa Yoshua wa Beth-shemeshi.

19. Basi BWANA aliwapiga baadhi ya watu wa Beth-shemeshi, kwa sababu wamechungulia ndani ya hilo sanduku la BWANA, wapata watu sabini, na watu hamsini elfu; nao watu wakalalamika, kwa kuwa BWANA amewapiga watu kwa uuaji mkuu.

20. Nao watu wa Beth-shemeshi wakasema, Ni nani awezaye kusimama mbele za BWANA, huyu Mungu mtakatifu? Naye atapanda kwenda kwa nani kutoka kwetu?

21. Nao wakatuma wajumbe waende kwa wenyeji wa Kiriath-yearimu, kusema, Wafilisti wamelirudisha sanduku la BWANA; basi shukeni, mkalichukue kwenu.

1 Sam. 6