2. Nao Wafilisti wakajipanga juu ya Israeli; na walipopigana, Israeli wakapigwa mbele ya Wafilisti; wakauawa watu wa jeshi lao lililokuwa uwandani wapata watu elfu nne.
3. Hata watu walipofika kambini, wazee wa Israeli wakasema, Mbona BWANA ametupiga leo mbele ya Wafilisti? Twende tukalilete sanduku la agano la BWANA toka Shilo hata huku, lije kati yetu, na kutuokoa katika mikono ya adui zetu.
4. Basi wakatuma watu kwenda Shilo, nao wakalileta toka huko sanduku la agano la BWANA wa majeshi, akaaye juu ya makerubi; na Hofni na Finehasi, wana wawili wa Eli, walikuwako huko pamoja na sanduku la agano la Mungu.
5. Na sanduku la agano la BWANA lilipoingia kambini, Israeli wote wakapiga kelele kwa sauti kuu, hata nchi ikavuma.
6. Nao Wafilisti waliposikia mshindo wa zile kelele, walisema, Maana yake nini mshindo wa kelele hizi kubwa katika kambi ya Waebrania? Wakatambua ya kuwa sanduku la BWANA limefika kambini.
7. Wafilisti wakaogopa, maana walisema, Mungu ameingia kambini. Wakasema, Ole wetu! Kwani halijawa jambo kama hili tangu hapo.
8. Ole wetu! Ni nani atakayetuokoa na mkono wa miungu hawa walio hodari? Hawa ndio miungu waliowapiga Wamisri kwa mapigo ya kila namna jangwani.
9. Iweni hodari, na kufanya kiume enyi Wafilisti, msije mkawa watumwa wa Waebrania, kama wao walivyokuwa watumwa wenu; fanyeni kiume, mkapigane nao.
10. Wafilisti wakapigana nao, Israeli wakapigwa, wakakimbia kila mtu hemani kwake; wakauawa watu wengi sana; maana katika Israeli walianguka watu thelathini elfu wenye kwenda vitani kwa miguu.
11. Hilo sanduku la Mungu Likatwaliwa; na Hofni na Finehasi, wale wana wawili wa Eli, wakauawa.
12. Basi, mtu mmoja wa Benyamini akapiga mbio kutoka mle jeshini akafika Shilo siku ile ile, hali nguo zake zimeraruliwa, na mavumbi kichwani mwake.
13. Alipofika, tazama, Eli alikuwa ameketi kitini pake kando ya njia, akingojea; maana moyo wake ulitetemeka kwa ajili ya sanduku la Mungu. Na yule mtu alipoingia mjini, akatoa habari, mji wote ukalia.
14. Naye Eli aliposikia kelele za kile kilio, akasema, Maana yake nini kelele za kishindo hiki? Yule mtu akafanya haraka, akaenda, akamwambia Eli.