1 Sam. 4:14-22 Swahili Union Version (SUV)

14. Naye Eli aliposikia kelele za kile kilio, akasema, Maana yake nini kelele za kishindo hiki? Yule mtu akafanya haraka, akaenda, akamwambia Eli.

15. Basi Eli umri wake umepata miaka tisini na minane; na macho yake yamepofuka hata asiweze kuona.

16. Yule mtu akamwambia Eli, Mimi ndimi niliyetoka jeshini, nami leo hivi nimekimbia toka jeshini. Naye akasema, Yalikwendaje, mwanangu?

17. Yeye aliyeleta habari akajibu, akasema, Israeli wamekimbia mbele ya Wafilisti, tena watu wengi sana wameuawa, hata na wana wako wawili, Hofni na Finehasi, wamekufa pia, na sanduku la Mungu limetwaliwa.

18. Ikawa alipolitaja sanduku la Mungu, Eli akaanguka kitini pake kwa nyuma, kando ya mlango, shingo yake ikavunjika, akafa; maana alikuwa mzee, tena mzito. Naye alikuwa amewaamua Israeli miaka arobaini.

19. Tena mkwewe, mkewe huyo Finehasi, alikuwa mja-mzito, karibu na kuzaa; basi, aliposikia habari ya kutwaliwa sanduku la Mungu, na ya kwamba mkwewe na mumewe wamekufa, akajiinamisha, akazaa; maana utungu wake ulimfikilia.

20. Hata alipokuwa katika kufa, wale wanawake waliohudhuria karibu naye wakamwambia, Usiogope; kwa maana umezaa mtoto mwanamume. Walakini hakujibu, wala hakumtazama.

21. Akamwita mtoto, Ikabodi, akisema, Huo utukufu umeondoka katika Israeli; kwa sababu sanduku la Mungu lilikuwa limetwaliwa, na kwa sababu ya mkwewe na mumewe.

22. Naam, akasema, Huo utukufu umeondoka katika Israeli; maana sanduku la Mungu limetwaliwa.

1 Sam. 4