1 Sam. 4:10-16 Swahili Union Version (SUV)

10. Wafilisti wakapigana nao, Israeli wakapigwa, wakakimbia kila mtu hemani kwake; wakauawa watu wengi sana; maana katika Israeli walianguka watu thelathini elfu wenye kwenda vitani kwa miguu.

11. Hilo sanduku la Mungu Likatwaliwa; na Hofni na Finehasi, wale wana wawili wa Eli, wakauawa.

12. Basi, mtu mmoja wa Benyamini akapiga mbio kutoka mle jeshini akafika Shilo siku ile ile, hali nguo zake zimeraruliwa, na mavumbi kichwani mwake.

13. Alipofika, tazama, Eli alikuwa ameketi kitini pake kando ya njia, akingojea; maana moyo wake ulitetemeka kwa ajili ya sanduku la Mungu. Na yule mtu alipoingia mjini, akatoa habari, mji wote ukalia.

14. Naye Eli aliposikia kelele za kile kilio, akasema, Maana yake nini kelele za kishindo hiki? Yule mtu akafanya haraka, akaenda, akamwambia Eli.

15. Basi Eli umri wake umepata miaka tisini na minane; na macho yake yamepofuka hata asiweze kuona.

16. Yule mtu akamwambia Eli, Mimi ndimi niliyetoka jeshini, nami leo hivi nimekimbia toka jeshini. Naye akasema, Yalikwendaje, mwanangu?

1 Sam. 4