1 Sam. 17:11-24 Swahili Union Version (SUV)

11. Basi Sauli na Israeli wote waliposikia maneno hayo ya Mfilisti, wakafadhaika na kuogopa sana.

12. Basi Daudi alikuwa mwana wa yule Mwefrathi, wa Bethlehemu ya Yuda, aliyeitwa jina lake Yese; naye huyo alikuwa na wana wanane; na yeye mwenyewe alikuwa mzee siku za Sauli, na mkongwe miongoni mwa watu.

13. Nao wale wana watatu wa Yese waliokuwa wakubwa walikuwa wamefuatana na Sauli kwenda vitani, na majina ya hao wanawe watatu waliokwenda vitani ni haya, mzaliwa wa kwanza Eliabu, na wa pili wake Abinadabu, na wa tatu Shama.

14. Naye huyo Daudi alikuwa mdogo wa wote; na hao watatu waliokuwa wakubwa wakafuatana na Sauli.

15. Basi Daudi alikuwa akienda kwa Sauli na kurudi ili awalishe kondoo za baba yake huko Bethlehemu.

16. Naye yule Mfilisti hukaribia asubuhi na jioni, akajitokeza siku arobaini.

17. Ndipo Yese akamwambia Daudi mwanawe, Haya! Sasa uwachukulie ndugu zako efa ya bisi, na mikate hii kumi, ipeleke upesi kambini kwa ndugu zako;

18. ukampelekee akida wa elfu yao jibini hizi kumi, ukawaangalie, wa hali gani, kisha uniletee jawabu yao.

19. Basi Sauli, na watu wote wa Israeli, walikuwa katika bonde la Ela, wakipigana na Wafilisti.

20. Daudi akaondoka asubuhi na mapema, akawaacha kondoo pamoja na mchungaji, akavitwaa vitu vile, akaenda, kama Yese alivyomwamuru; akafika penye magari, wakati lile jeshi walipokuwa wakitoka kwenda kupigana, wakipiga kelele za vita.

21. Nao Waisraeli na Wafilisti wakajipanga, jeshi hili likikabili jeshi hili.

22. Basi Daudi akaviacha vile vyombo vyake katika mkono wa mlinda vyombo, akalikimbilia jeshi, akafika, akawasalimu ndugu zake.

23. Hata alipokuwa akisema nao, kumbe! Yule shujaa alitokea, yule Mfilisti wa Gathi, jina lake Goliathi, akitoka katika jeshi la Wafilisti, akasema maneno yale yale; naye Daudi akayasikia.

24. Na watu wote wa Israeli walipomwona yule mtu wakakimbia, wakaogopa sana.

1 Sam. 17