4. Ndipo Sauli akawaita watu, akawahesabu huko Telemu, askari waliopanda farasi mia mbili elfu, na watu wa Yuda kumi elfu.
5. Sauli akaufikilia mji wa Amaleki, akauvizia bondeni.
6. Sauli akawaambia Wakeni, Haya! Enendeni zenu, mkashuke ili kujitenga na Waamaleki, nisije nikawaangamiza ninyi pamoja nao; maana mliwatendea wana wa Israeli mema, walipopanda kutoka Misri. Basi hao Wakeni wakaondoka, wakajitenga na Waamaleki.
7. Sauli akawapiga Waamaleki, toka Havila uendapo Shuri, unaokabili Misri.
8. Akamkamata Agagi, mfalme wa Waamaleki, yu hai, akawaangamiza hao watu wote kwa upanga.
9. Lakini Sauli na watu wake wakamwacha Agagi hai, na katika kondoo walio wazuri, na ng’ombe, na vinono, na wana-kondoo, na cho chote kilicho chema, wala hawakukubali kuwaangamiza; bali cho chote kilichokuwa kibaya na kibovu, ndicho walichokiangamiza kabisa.
10. Ndipo neno la BWANA likamjia Samweli, kusema,
11. Najuta kwa sababu nimemtawaza Sauli awe mfalme; maana amerudi nyuma, asinifuate, wala hakufanya nilivyomwamuru. Samweli akasikitika, akamlilia BWANA usiku kucha.
12. Samweli akaondoka asubuhi na mapema ili aonane na Sauli; Samweli akaambiwa ya kwamba, Sauli alifika Karmeli, na tazama, akajisimamishia ukumbusho, akageuka, akapita, akatelemkia Gilgali.
13. Samweli akamwendea Sauli; naye Sauli akamwambia, Ubarikiwe na BWANA, nimeitimiza amri ya BWANA.
14. Samweli akasema, Maana yake nini, basi, hiki kilio cha kondoo masikioni mwangu, na huu mlio wa ng’ombe ninaousikia?
15. Sauli akasema, Wamewaleta kutoka kwa Waamaleki; maana watu waliwaacha hai kondoo na ng’ombe walio wazuri, ili wawatoe dhabihu kwa BWANA, Mungu wako, nao waliosalia tumewaangamiza kabisa.
16. Ndipo Samweli akamwambia Sauli, Ngoja, nami nitakuambia neno aliloniambia BWANA usiku huu. Naye akamwambia, Haya, sema.