25. Basi sasa, nakuomba, unisamehe dhambi yangu; rudi pamoja nami, nipate kumwabudu BWANA.
26. Samweli akasema, Sitarudi pamoja nawe; kwa sababu umelikataa neno la BWANA, BWANA naye amekukataa wewe, usiwe mfalme wa Israeli.
27. Naye Samweli alipogeuka, aende zake, Sauli akaushika upindo wa vazi lake, nalo likararuka.
28. Basi Samweli akamwambia, Leo BWANA amekurarulia ufalme wa Israeli, naye amempa jirani yako, aliye mwema kuliko wewe.
29. Tena Yeye aliye Nguvu za Israeli hatanena uongo, wala hataona majuto; maana siye mwanadamu, hata ajute.
30. Akasema, Nimekosa; lakini uniheshimu sasa, nakuomba, mbele ya wazee wa watu wangu, na mbele ya Israeli, rudi pamoja nami, nimwabudu BWANA, Mungu wako.
31. Basi Samweli akarudi na kuandamana na Sauli; naye Sauli akamwabudu BWANA.
32. Ndipo Samweli akasema, Nileteeni hapa Agagi, mfalme wa Waamaleki. Basi Agagi akamwendea kwa utepetevu. Naye Agagi akasema, Bila shaka uchungu wa mauti umeondoka.
33. Lakini Samweli akamjibu, Kama upanga wako ulivyofanya wanawake kufiwa na watoto wao, vivyo hivyo mama yako atafiwa miongoni mwa wanawake. Basi Samweli akamkata Agagi vipande mbele za BWANA huko Gilgali.
34. Na baada ya hayo Samweli akaenda zake kule Rama; naye Sauli akakwea kwenda nyumbani kwake huko Gibea ya Sauli.
35. Wala Samweli hakuenda tena kuonana na Sauli hata siku ya kufa kwake; lakini Samweli alikuwa akimlilia Sauli; naye BWANA akaghairi ya kuwa amemtawaza Sauli awe mfalme juu ya Israeli.