10. Ndipo neno la BWANA likamjia Samweli, kusema,
11. Najuta kwa sababu nimemtawaza Sauli awe mfalme; maana amerudi nyuma, asinifuate, wala hakufanya nilivyomwamuru. Samweli akasikitika, akamlilia BWANA usiku kucha.
12. Samweli akaondoka asubuhi na mapema ili aonane na Sauli; Samweli akaambiwa ya kwamba, Sauli alifika Karmeli, na tazama, akajisimamishia ukumbusho, akageuka, akapita, akatelemkia Gilgali.
13. Samweli akamwendea Sauli; naye Sauli akamwambia, Ubarikiwe na BWANA, nimeitimiza amri ya BWANA.
14. Samweli akasema, Maana yake nini, basi, hiki kilio cha kondoo masikioni mwangu, na huu mlio wa ng’ombe ninaousikia?
15. Sauli akasema, Wamewaleta kutoka kwa Waamaleki; maana watu waliwaacha hai kondoo na ng’ombe walio wazuri, ili wawatoe dhabihu kwa BWANA, Mungu wako, nao waliosalia tumewaangamiza kabisa.
16. Ndipo Samweli akamwambia Sauli, Ngoja, nami nitakuambia neno aliloniambia BWANA usiku huu. Naye akamwambia, Haya, sema.
17. Basi Samweli akasema, Ingawa ulikuwa mdogo machoni pako mwenyewe, je! Hukufanywa kuwa kichwa cha kabila za Israeli? Naye BWANA akakutia mafuta uwe mfalme wa Israeli.
18. Kisha BWANA akakutuma safarini, akasema, Enenda ukawaangamize kabisa wale Waamaleki wenye dhambi, upigane nao hata watakapoangamia.
19. Mbona, basi, hukuitii sauti ya BWANA, bali ukazirukia nyara ukafanya yaliyo maovu machoni pa BWANA?