1. Wakati huo Samweli akamwambia Sauli, BWANA alinipeleka nikutie mafuta, uwe mfalme wa watu wake Israeli; basi sasa, isikilize sauti na maneno ya BWANA.
2. BWANA wa majeshi asema hivi, Nimeyatia moyoni mwangu mambo hayo Amaleki waliyowatenda Israeli, jinsi walivyowapinga njiani, hapo walipopanda kutoka Misri.
3. Basi sasa enda ukawapige Amaleki, na kuviharibu kabisa vitu vyote walivyo navyo, wala msiwaachilie; bali waueni, mwanamume na mwanamke, mtoto naye anyonyaye, ng’ombe na kondoo, ngamia na punda.
4. Ndipo Sauli akawaita watu, akawahesabu huko Telemu, askari waliopanda farasi mia mbili elfu, na watu wa Yuda kumi elfu.
5. Sauli akaufikilia mji wa Amaleki, akauvizia bondeni.
6. Sauli akawaambia Wakeni, Haya! Enendeni zenu, mkashuke ili kujitenga na Waamaleki, nisije nikawaangamiza ninyi pamoja nao; maana mliwatendea wana wa Israeli mema, walipopanda kutoka Misri. Basi hao Wakeni wakaondoka, wakajitenga na Waamaleki.
7. Sauli akawapiga Waamaleki, toka Havila uendapo Shuri, unaokabili Misri.
8. Akamkamata Agagi, mfalme wa Waamaleki, yu hai, akawaangamiza hao watu wote kwa upanga.