1. Kisha Samweli akawaambia Israeli wote, Angalieni, nimeisikiliza sauti yenu katika hayo yote mliyoniambia, nami nimemtawaza mfalme juu yenu.
2. Basi sasa, angalieni, mfalme anakwenda mbele yenu; na mimi ni mzee, mwenye mvi; tena, tazameni, wana wangu wapo pamoja nanyi; nami nimekwenda mbele yenu toka ujana wangu hata leo.
3. Nami nipo hapa; basi, mnishuhudie mbele za BWANA, na mbele ya masihi wake, nalitwaa ng’ombe wa nani? Au nalitwaa punda wa nani? Au ni nani niliyemdhulumu? Ni nani niliyemwonea? Au kwa mkono wa nani nimepokea rushwa inipofushe macho? Nami nitawarudishia ninyi.
4. Nao wakasema, hukutudhulumu, wala hukutuonea, wala hukupokea kitu kwa mkono wa mtu awaye yote.