1 Sam. 10:5-15 Swahili Union Version (SUV)

5. Baada ya hayo utafika Gibea ya Mungu, hapo palipo na ngome ya Wafilisti; kisha itakuwa, utakapofika mjini, utakutana na kundi la manabii wakishuka kutoka mahali pa juu, wenye kinanda, na tari, na kinubi, na filimbi mbele yao, nao watakuwa wakitabiri;

6. na roho ya BWANA itakujilia kwa nguvu, nawe utatabiri pamoja nao, nawe utageuzwa kuwa mtu mwingine.

7. Basi, hapo ishara hizi zitakapokutukia, fanya kama uonavyo vema; kwa kuwa Mungu yu pamoja nawe.

8. Nawe utatelemka mbele yangu mpaka Gilgali; nami, angalia, nitakutelemkia huko, ili kutoa sadaka za kuteketezwa, na kuchinja sadaka za amani; siku saba utangoja, hata nitakapokujia, na kukuonyesha yatakayokupasa kuyafanya.

9. Ikawa, alipogeuka kumwacha Samweli, Mungu akambadilisha moyo; nazo ishara zile zote zikatukia siku ile ile.

10. Basi, walipofika Gibea, tazama, kikosi cha manabii wakakutana naye; kisha roho ya Mungu ikamjilia kwa nguvu, naye akatabiri kati yao.

11. Ikawa, wote waliomjua zamani walipoliona jambo hilo, kwamba, tazama, huyo anatabiri pamoja na manabii, ndipo watu wakasemezana, Ni nini hilo lililompata mwana wa Kishi? Je! Sauli pia yumo miongoni mwa manabii?

12. Naye akajibu mtu mmoja wa mahali hapo, akasema, Na baba yao n’nani? Kwa hiyo ikawa mithali, Je! Sauli pia yumo miongoni mwa manabii?

13. Naye alipokwisha kutabiri, alipafikilia mahali pale pa juu.

14. Basi babaye mdogo akamwuliza Sauli na mtumishi wake, Je! Mlikwenda wapi? Naye akajibu, Tulikwenda ili kuwatafuta hao punda; na tulipoona ya kwamba hawakuonekana, tulimwendea Samweli.

15. Babaye mdogo Sauli akasema, Tafadhali uniambie, huyo Samweli aliwaambiaje?

1 Sam. 10